Joyce Anael, Moshi
Anne Makinda |
MWENYEKITI wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda, amezitaka hospitali na vituo vya afya vya
umma kutoa huduma bora ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zina vifaatiba na dawa.
Makinda alitoa rai hiyo jana kwenye
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro mjini hapa akisema watu binafsi wamekuwa
wakinufaika na fedha za huduma ambazo zinatolewa na NHIF kutokana na vituo vya umma
kushindwa kutoa huduma nzuri na bora.
Alisema ipo haja sasa Serikali
kuhakikisha kuna vifaa vya kutosha kwenye vituo vya afya na hospitali za
Serikali, ili kutoa huduma bora na nzuri na kuvutia wananchi wengi zaidi.
"Hospitali za umma ni za muda
mrefu, majengo yapo hivyo wanaweza kutoa huduma bora na wananchi wakaenda huko,
ni suala tu la kujipanga," alisema.
Alisema watu binafsi wamekuwa
wakichangamkia fursa za NHIF kwa kutoa huduma nzuri na bora, na kufanya
wananchi kukimbilia huko badala ya vituo vya umma ambavyo vimeonekana kushindwa kutoa huduma nzuri.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard
Konga alisema fedha nyingi zinazotoka katika mfuko huo, zimekwenda vituo
binafsi na maduka ya dawa ya binafsi, licha ya Serikali kuwa na vituo vingi na
hospitali nyingi nchini hususan vijijini.
Alisema tatizo kubwa katika vituo na
hospitali za Serikali kwa sasa ni upungufu wa dawa, hivyo kuna haja ya kuliangalia
suala hilo kwa makini na kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya dawa zinatumika
kwa ajili ya dawa badala ya kupelekwa kwenye maeneo mengine.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi
Sadick aliiomba NHIF kufuatilia mkopo ulioombwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
huo, wa Mawenzi kwa ajili ya kujenga
duka la dawa na kuuwezesha kutoka, hatua ambayo itasaidia kupunguza adha ya
wagonjwa kwenda kununua dawa kwa gharama kubwa katika maduka ya dawa ya
binafsi.
0 comments:
Post a Comment