Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza
kufurahishwa na uamuzi wa Kanisa Katoliki na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT)
kutafuta viwanja Dodoma ili kujenga ofisi za makao yao makuu na makazi ya
viongozi wao wakuu.
Alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na
Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya na Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC), Peter Maduki ofisini
kwake Dodoma.
“Sina shaka juu ya maombi yenu ya kupewa
viwanja kujenga makao makuu na makazi ya viongozi wakuu. Sasa hivi mpango wa Dodoma kama makao makuu ya
nchi inapitiwa upya, ili izingatie mahitaji ya msingi kwa sababu zamani ilikuwa
haijapangwa kwa mazingira ya sasa ya ujio wa Serikali,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema wiki tatu zilizopita, alimwagiza
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) atafute kampuni
zenye uwezo wa kupima viwanja haraka.
“Hii itatusaidia kutambua tuna eneo
kiasi gani na mahitaji halisi ni yapi na nani akija apewe eneo lipi kulingana
na mahitaji yake,” aliongeza.
Awali Askofu Kinyaiya alimweleza Waziri
Mkuu kwamba wanahitaji eneo la kujenga ofisi za makao makuu na makazi kwa ajili
ya Kanisa na makanisa yaliyo chini ya CCT ambayo kwa pamoja yanaunda Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii
(CSSC).
Alisema wanahitaji eneo kwa ajili ya
ujenzi wa ofisi, pia makazi ya Balozi wa Baba Mtakatifu nchini.
Alisema walipowasilisha maombi yao CDA,
waliahidiwa kupewa eneo la makazi tu, lakini bado wanahitaji eneo la ofisi.
Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru
Waziri Mkuu kwa alivyoiwakilisha Serikali kwenye maziko ya Mhashamu Askofu mstaafu Mathias Isuja
wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dodoma ambaye alifariki dunia Aprili 13 na
kuzikwa Aprili 20.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alishukuru makanisa kwa
huduma za kijamii zitolewazo katika sekta za elimu, afya na kilimo kama
alivyoshuhudia katika baadhi ya maeneo nchini.
Pia aliwakubalia maombi ya kikao cha
pamoja baina ya watendaji wa Serikali na makanisa ambacho kitajadili namna ya
kuimarisha ubia katika utoaji wa huduma za kijamii hususan kwenye afya na
elimu.
“Kikao hiki kitafanya mapitio ya huduma
zinazotolewa baina ya Serikali na Makanisa, lakini pia kitatusaidia kupata
mrejesho wa mambo yanayofanyika kwenye hospitali na shule mnazomiliki katika
maeneo mbalimbali nchini,” aliongeza.
Alitaka waharakishe kuleta mapendekezo
yao ili kikao hicho kifanyike kabla ya Desemba, mwaka huu, kwani kitaisaidia
Serikali kupata mrejesho wa kuboresha baadhi ya maeneo katika mwaka mpya wa
kielimu unaoanza Januari kila mwaka.
Katika
mkutano huo, Maduki alisema katika sekta ya afya
hadi Juni, makanisa yalikuwa yanamiliki na kuendesha hospitali 102, vituo vya
afya 102 na zahanati 696.
“Kati ya hospitali 102, mbili ni za
rufaa za kanda na 38 ni za hospitali teule za halmashauri za wilaya na
hospitali zingine 62 zinatoa huduma halmashauri mbalimbali,” alisema.
Alisema karibu asilimia 38 ya hospitali
nchini zinamilikiwa na makanisa na nyingi ziko maeneo ya vijijini. Pia alisema
kuna chuo kikuu kimoja, vyuo vikuu vishiriki vitatu, na vyuo vya mafunzo ya
kati 62 ambavyo vinatoa kozi za uuguzi, maabara na ufamasia.
Kuhusu sekta ya elimu, Maduki alisema
makanisa yanatoa elimu kuanzia ya awali hadi chuo kikuu na kwamba hadi kufikia
Juni, 2016, makanisa yalikuwa na shule za msingi 161, za sekondari 369, na vyuo
vya ufundi stadi 126.
“Pia tuna vyuo vya ualimu 14, vyuo vikuu
tisa, vyuo vikuu vishiriki 17 na vituo vya vyuo vikuu saba,” alisema.
0 comments:
Post a Comment