Salha Mohamed
WANAFUNZI 12 wa vyuo vikuu nchini
wanatarajia kwenda Ghana kujifunza na kuongeza uwezo kwenye masoko ya dhamana
na mitaji.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam juzi kwenye
hafla ya utoaji tuzo kwa washindi wa masoko ya dhamana na mitaji ulioshirikisha
wanafunzi 7,791 wa vyuo vikuu vya nchini huku walioshinda nafasi hizo, wakiwa ni
80 pekee.
Akizungumza baada ya mchakato wa kupata
washindi wa tuzo hizo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji
alisema wanafunzi waliofaulu tuzo hizo watakuwa mabalozi wazuri wanakokwenda
kujifunza.
"Kwenda kwenu Ghana kutasaidia kuwajengea
uwezo washiriki wote katika soko la mitaji ... mkirudi muwe mabalozi wazuri wa kufundisha
wengine elimu hiyo nchi nzima," alisema.
Alisema mwaka jana wanafunzi hao
walikwenda Afrika Kusini, na Serikali iliahidi kuwakwamua watakapokwama.
"Nitoe rai kwa mamlaka hii
kuwafikia wananchi na kueleza umuhimu kwa jamii ili kutanua huduma mnayotoa,
lakini pia mamlaka kukubaliana na changamoto kwa kutoa elimu na kujenga uwezo
ili kuongeza hamasa," alisema.
Aliongeza kuwa kupata ujuzi huo
kutapunguza idadi ya wananchi wanaokaa mitaani kwani watajiajiri na kuongeza
pato la Taifa kwa asilimia 7.
Alisema ni vema vijana hao wakajengewa
uwezo na kujiamini kuzungumza mbele za watu na kwamba mashindano mengine yatashirikisha
walimu wa sekondari.
Mshindi wa kwanza alipata Sh milioni
1.8, wa pili Sh milioni 1.4 wa tatu
wakichukua Sh 500,000 na wa nne na wa tano wakishinda Sh 200,000 kila mmoja.
Washindi hao walitoka vyuo vikuu vya Ardhi,
Dar es Salaam (UDSM), Mzumbe, Dodoma (UDOM), cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na
Chuo cha Uhasibu (TIA).
0 comments:
Post a Comment