Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba kuifanyia marekebisho
makubwa Bodi ya Korosho na Menejimenti yake,
baada ya kushindwa kusimamia zao hilo ipasavyo.
Amesema Serikali itafanya mapitio ya
bodi zote za mazao ya biashara na imeanza na korosho baadaye pamba, tumbaku,
kahawa, katani na chai. Katika tathmini na mapitio hayo, bodi itakayobainika
kushindwa kutekeleza majukumu yake itavunjwa.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi alipohutubia
wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja cha Sokoine
wilayani Nachingwea mkoani Lindi.
Aliishangaa bodi hiyo kuacha kutekeleza
majukumu yake na kuingilia minada ya korosho na kuzuia baadhi ya
wafanyabiashara kununua zao hilo hali inayoashiria kuwapo watu waliopangwa
kununua bila ya utaratibu.
“Bodi leo wamejipa jukumu la kusimamia
minada! Si kazi yao ni ya chama kikuu, korosho inalimwa kuanzia Ruvuma hadi
Tanga, mtasimamia minada mingapi? Viachieni vyama vikuu.
“Vyama vikuu vikiharibu walalamikaji
waje kwenu kama sehemu ya rufaa. Ninyi mnasimamia minada mnaharibu, walalamikaji
watakwenda kwa nani? Kwa nini mng’ang’anie
kwenda kwenye minada?” Alihoji Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisema Ijumaa bodi hiyo
ilisitisha mnada wa korosho Lindi kwa sababu wanunuzi hawakuweka dhamana ya
mauzo na alishatoa maagizo ya kutaka wanunuzi wasiruhusiwe kununua hadi waweke
asilimia 25 ya malipo.
Alisema maagizo hayo aliyatoa tangu Aprili
ila watendaji wa bodi hiyo
hawakuyafanyia kazi kwa wakati na badala yake walizuia wafanyabiashara
waliotaka kununua korosho Lindi kwa madai ya kutokuwa na bondi huku wakiruhusu
wa Mtwara.
“Kama kule walinunua bila bondi kwa nini
wasiruhusu na Lindi wakanunua bila bondi ili nijue kwamba mliamua kugoma kutekeleza
maelekezo ya Serikali? Au hamkumtaka aliyeshinda nyie
mlikuwa mnamtaka nani? Nitashughulika nanyi,” alisisitiza.
Aliongeza: “Nimesema tukitoa maelekezo
lazima yatekelezwe na atakayeshindwa hatufai, Mheshimiwa Mbunge umelalamika juu
ya Bodi, hawa ndio wabeba maelekezo, hatujawahi kuona bodi ya korosho ikienda
vijijini kuzungumza na vyama vikuu hata mara moja.”
Akizungumzia suala la wakulima
kulazimishwa kufungua akaunti za
kupitishia malipo yao alisema wasiwalazimishe. “Waelimisheni wakulima umuhimu
wa kufungua akaunti, lakini si kwa kuwalazimisha wote wawe na akaunti hadi yule
mwenye kilo tano…na akaunti yenyewe inafunguliwa kwa Sh 100,000,” alisema.
Alisema: “Wanashindwa kutekeleza
niliyowaagiza, halafu wanasingizia utendaji wao mbovu kuwa ndio maagizo yangu,
niliwaagiza wapi?” Alihoji na kuongeza: “Yapo makundi yanafanya mambo
yanavyotaka halafu yakiwazidi mambo wanasingizia viongozi wa juu na ndio wale
wanaosema kila kitu nimeagizwa kutoka juu, juu wapi?
“Lazima tuendelee kudhibiti nidhamu ya
vyombo tunavyounda kwa ajili ya kuhudumia wananchi. Tutaendelea kusimamia
nidhamu kwa taasisi zinazohudumia wakulima nchi nzima,” alisisitiza.
Wakati
huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi
alimkabidhi Waziri Mkuu msaada wa Sh milioni 16.3 pamoja na nguo kwa ajili ya
kusaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
0 comments:
Post a Comment