Tuipe mkazo taaluma ya ualimu tuinue elimu nchini


Salha Mohamed

TAFITI zinaonesha kuwa nchi nyingi zinazopiga hatua kubwa katika maendeledo ya uchumi ni zile ambazo zimewekeza katika elimu bora kwa wananchi walio wengi.

Elimu inayotolewa nchini haimjengi mwanafunzi kuweza kujiajiri au kujitoa katika ujinga aliokuwa nao kwa maana haimkomboi mwanafunzi.

Kama ambavyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako anakiri kuangalia upya sifa za walimu kwani mwalimu ndiyo chachu ya kuwa na wanafunzi bora.

Walimu hao pia wanapaswa kuwa na uwezo mkubwa ili kuongeza uwezo katika kufundisha wanafunzi.

Uwezo huo utakaokuza na kuongeza maarifa katika jamii zao na kuwatoa katika umasikini kwa kuwaongezea maarifa ikiwa ni pamoja na kujiajiri.

“Kama wizara hatuwezi kurudi nyuma katika hilo, katika masomo anayotaka kuyachukua mwalimu awe amefaulu si chini ya alama C, lakini tungetamani sana wale waliopata daraja A,” anasema.

Anasema bado wanaimarisha mifumo ya elimu, ili iwe mizuri zaidi kwa kuangalia sifa za walimu kulingana na wakati, kwani wanaamini kuwa mwalimu anapokuwa na uwezo mkubwa anaweza kuwafundisha kwa weledi zaidi wanafunzi wake.

Pia anaeleza kuwa pindi wanapobaini walimu wamedahiliwa kimakosa na vyuo hatua zimekuwa zikichukuliwa.

“Sifa za mwalimu anapokwenda kusoma lazima awe na daraja C mbili katika masomo atakayofundisha,” anasema Profesa Ndalichako.

Kutokana na hali hiyo, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anasema tafiti zinaonesha kwamba ili kuboresha ubora wa elimu kitu kikubwa na cha msingi kabisa kuliko vyote ni kuwekeza kwa walimu na taaluma ya ualimu.

Anasema maeneo muhimu ni mafunzo ya walimu na kuhakikisha wanakuwa na motisha ya kutosha katika kufanya kazi zao.

“Bahati mbaya hapa Tanzania, serikali na jamii kwa ujumla hatuthamini kazi ya ualimu. Taaluma ya ualimu imekuwa ni daraja la kujiokoa baada ya kukosa sehemu zingine.

“Walimu wetu wanaofundisha katika mazingira magumu sana hatuwathamini na wakati mwingine hata tunawabeza,” anasema Zitto.

Pia anasema kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi unaonesha kuwa walimu ndio msingi mkuu wa kujifunza na kuboresha elimu.

Na kwamba chama chake kinasisitiza kuwekeza katika mafunzo ya walimu na kuhakikisha walimu  wanalipwa kwa kiwango ambacho kitawawezesha kukabiliana na maisha huko walipo.

Zitto anasema bado tafiti zinaonesha kwamba walimu walio vijijini wanaishi katika maisha magumu sana hasa ya kukosa makazi yenye staha.

“Ili kuwa na utatuzi endelevu wa matatizo ya walimu na kuchochea motisha ya kujiunga na taaluma ya ualimu, chama chetu kinapendekeza tuwe na mfumo mpya maalumu wa ajira ya walimu katika utumishi wa umma,” anasema.

Anasema hali hiyo ni muhimu kwani takribani nusu ya watumishi wote wa umma wapo katika sekta ya elimu, na kwamba hatua hiyo itawezesha kuwa na bajeti maalumu ya walimu.

Kwani tafiti zinaonesha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanaopita katika mfumo wa elimu Tanzania wanamaliza shule wakiwa mbumbumbu.

Hii inadhihirisha kutokuwa na ubora wa upatikanaji wa walimu nchini ndivyo ambavyo matokeo ya wanafunzi hao yanakuwa mabaya.

Zitto anasema kuwa miaka kadhaa utafiki uliofanywa na wa Shirika la Uwezo unaonesha, watoto watatu kati ya 10 wa Darasa la Tatu hawawezi kumudu kufanya hesabu ya darasa la pili.

Na kwamba mwanafunzi mmoja kati ya wanne asilimia 25 waliopo darasa la saba hawawezi kufanya hesabu ya darasa la pili.

Anasema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, chini ya asilimia 10 ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wanafaulu kwa kiwango cha daraja la I hadi la III.

“Ndiyo kusema asilimia 90 wanapata daraja la nne au wanafeli. Kwa mfumo wetu wa elimu hawa hawawezi kuendelea na ngazi yoyote rasmi ya elimu,” anasema.

Anasema kutokana na udhaifu katika elimu ya ufundi ina maana kuwa wanaingia mitaani wakiwa hawana maarifa na stadi muhimu za kujiajiri au kuajiriwa.

Mbunge huyo wa Kigomba Mjini, anasema hatua nyingi ambazo serikali inachukua katika sekta ya elimu zinalenga katika kuongeza idadi ya wanafunzi, lakini si kuboresha ubora wa elimu.

“Tumesikia sana kauli kuhusu elimu bure. Tumesikia sana kuhusu kuongeza madawati. Pamoja na umuhimu wake, ukweli ni kwamba hatua hizi hazitasaidia kuongeza kiwango cha ubora wa elimu yetu,” anasema.

Kwa upande wake, Mahamudu Ally ambaye ni mmoja wa wazazi wa mwanafunzi anayesoma Shule  ya Msingi Kipunguni jijini Dar es Salaam ambayo imefanya vibaya katika mtihani wa moko kwa darasa la nne uliofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu, anasema katika kata hiyo yenye shule 10 shule za serikali ni mbili ambazo hazijafanya vema katika mtihani huo.

Anasema shule za serikali hasa za msingi zimekuwa zikifanya vibaya dhidi ya shule za watu binafsi katika mitihani ya moko na hata darasa la saba.

“Hali hiyo inasababishwa na walimu kushindwa kujitoa katika kufundisha na badala yake kutaka wanafunzi kusoma masomo ya ziada kwa kiasi fulani cha malipo,” anasema Ally.

Anatoa mwito kwa walimu kufundisha kwa nguvu zao zote ili kuwasaidia vijana wa Tanzania nao wafikie malengo yao. Na pia anaishauri Serikali kutatua kero mbalimbali zinazowakabili walimu nchini.

Hivyo kama ambavyo serikali imeahidi kutoa elimu bora kwa wanafunzi hapa nchini ni lazima kuandaliwe mazingira mazuri ya kupatikana kwa walimu bora.

Walimu hao watakaokuwa na uwezo wa kufundisha wanafunzi na kuwajengea uwezo na wa kuweza kufikia malengo yao na si kuongeza idadi ya watoto wa mitaani.

Pia kuzalisha watoto watakaokuwa tayari kujiajiri na si kutegemea kuajiriwa na kuweza kusaidia jamii zao kichumi.

Ninaamini kuwa kama serikali italiangalia hilo litaweza kupunguza idadi ya watoto wa mitaani pamoja na jamii isiyokuwa na kazi na kusababisha kuwa na wimbi kubwa la wategemezi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo