Joyce Kasiki, Dodoma
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan
amesema Serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 70 za kununua dawa na vifaatiba
ili kumaliza tatizo la ukosefu wa dawa nchini.
Pia
imetenga Sh bilioni 85 za kupunguza deni linalodaiwa na Bohari Kuu ya Dawa
(MSD) ili Bohari hiyo itoe huduma bora ya dawa kwa wananchi.
Akifungua mkutano mkuu wa waganga wakuu
wa mikoa na wilaya zote nchini jana
mjini hapa, Samia alisema dawa hizo zitakazonunuliwa zitakwenda moja kwa moja kwenye vituo vya afya nchini.
Alisema lengo la Serikali ni kupunguza
changamoto zilizo kwenye sekta ya afya, huku akiweka bayana dhamira ya Serikali
ya kujenga kiwanda cha dawa mkoani Simiyu.
“Kwa mwaka huu tumepanga kwenye bajeti Sh
bilioni 85 ambazo tutapunguzia deni la MSD ili iweze kutoa dawa kwa hospitali
zetu,
“Lakini pia tumetenga Sh bilioni 70 kwa
ajili ya kupeleka dawa vituoni, lakini ninyi mna ya kwenu, hata pale mnapokuwa
na pesa mna hiari mwende kwenye maduka binafsi, lakini MSD nao wana yao, tutakaa
nao tuseme nao, wahakikishe dawa zinazotakiwa zipo kwenye MSD,”alisema.
Mbali na hilo, alizungumzia suala la
tiba asili na mbadala na kuitaka Wizara ya Afya, kuhakikisha inazitambua dawa
hizo na kuzisajili.
“Tunapaswa tuzijue na tuzifanyie utafiti
dawa za asili, tukiridhika na utafiti kwamba dawa inatibu kitu fulani, basi
tuisajili, tusajili anayeshughulikia
dawa yenyewe na kuona jinsi tutakavyoiendeleza.
“Tiba asili na mbadala zina umuhimu,
kama tunavyojua tuna upungufu mkubwa katika sekta ya afya hasa vijijini,
zinazotusaidia ni tiba asili, naomba tuzipe umuhimu,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa Waganga hao, Dk Sudi
Leonard alisema ukosefu wa dawa na vifaa tiba kwenye baadhi ya vituo vya afya
nchini unasababisha malalamiko kwa wananchi kutokana na mchakato mrefu wa
upatikanaji wa dawa hizo kutoka MSD.
“Kwa sasa maombi yetu ya dawa hupatikana
kwa asilimia 40 hadi 55 na zinazokosekana inatulazimu kununua nje ya MSD,”
alisema Dk Leonard.
Mkutano huo ni wa siku nne ambao ulishirikisha
waganga wakuu wa mikoa na wilaya na wauguzi, lengo likiwa ni kujadili masuala yahusuyo
sekta ya afya zikiwamo changamoto na namna ya kuzitatua.
0 comments:
Post a Comment