Hussein Ndubikile
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema
wanafunzi wote wa elimu ya juu wanaostahili mikopo watapewa ndani ya saa 72
kuanzia jana.
Pia amebainisha kuwa Serikali imeongeza
kiwango cha bajeti ya mikopo kutoka Sh bilioni 340 hadi Sh bilioni 483 kwa
mwaka wa fedha 2016/17.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana katika
kilele cha Maadhimisho ya Miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu
kilipoanzishwa Oktoba 25, 1961.
Alisema kuanzia juzi Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini, ilianza kuwapa mikopo wanafunzi wachache huku
akisisitiza kuwa kufikia kesho asilimia 90 ya wanafunzi wanaostahiki mikopo
watapewa.
"Wachache sana jana (juzi) walianza
kupewa mikopo, kufikia keshokutwa (kesho) Serikali itawapa mikopo asilimia 90
ya wanaotakiwa kupata," alisema.
Majaliwa alisema Serikali haitavumilia
ucheleweshaji wa makusudi wa fedha utakaofanywa na Mamlaka husika, huku
akieleza taasisi za elimu kufikisha taarifa sehemu husika ili kuepuka migogoro
ya wanafunzi na Serikali yao.
Aliongeza kuwa hadi Oktoba 20 Serikali
ilifanya uhakiki wa wafanyakazi 16,500 na baada ya mchakato huo uhakiki wa
malimbikizo ya madeni ya watumishi wa chuo hicho utafanyika ili walipwe stahiki
zao kwa wakati.
Alisema Serikali itaendelea kuajiri
watumishi wakiwamo wahadhiri waandamizi watakapohitajika na kuongeza ukusanyaji
wa mapato ya ndani ili kusaidia uendeshaji wa taasisi za umma.
Alifafanua kuwa Serikali imeshaonesha
nia ya dhati ya kukabiliana na changamoto za miundombinu zinazokikabili chuo
hicho, ikiwamo mahali pa kulala wanafunzi, vitendea kazi vya maabara kwa kuanza
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni 3,840 unaoendelea.
Alipongeza mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere na Baraza lake la Mawaziri kwa kufanikisha kuanzishwa chuo
hicho, lengo lake likiwa ni kupambana na changamoto za ujinga, maradhi na umasikini.
Pia katika maadhimisho hayo, Waziri
Majaliwa alizindua kitabu cha Lumumba Street To the Hill and Beyond
kinachoelezea jinsi chuo kilivyoanzishwa, maono na viongozi walioshiriki
kukianzisha.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,
Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema Sh
bilioni tisa zimetengwa na Wizara kushughulikia matatizo ya miundombinu ya chuo
hicho na mchakato wa kuhakikisha fedha zinapatikana unaendelea.
Dk Akwilapo alisema ujenzi wa mabweni
utakamilika mwishoni mwa mwaka, huku akibainisha kuwa yatapokamilika
yatapunguza tatizo la malazi kwa kiasi kikubwa.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa
Rwekaza Mukandala alisema chuo kilianza na udahili wa wanafunzi wachache ambapo
sasa kinadahaili zaidi ya wanafuzi 13,000,
hivyo tangu kianzishwe kimetoa mchango mkubwa wa kuzalisha wanataaluma 90,000
walio serikalini na taasisi binafsi.
Alisema licha ya Serikali kuendelea kuzifanyia
kazi changamoto zinazokikabili bado kina uhaba wa rasilimaliwatu kutokana na
usitishwaji wa ajira, malimbikizo ya madeni ya watumishi, vitendea kazi vya
maabara na uhaba wa wahadhiri waandamizi.
Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba
ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa mwanzoni wa chuo hicho, alisema wakati akiwa
chuoni hapo masomo yaliyokuwa yakifundishwa yalikuwa machache na miundombinu ya
majengo michache, huku akikipongeza kwa kufanya juhudi za dhati kuzalisha
wasomi wanaolitumikia Taifa.
Mwanasheria na Katibu wa Chuo hicho,
Profesa Palamagamba Kabudi alisema chuo kilianza na wafanyakazi sita na
wanafunzi 14 wakiwamo Peter Kilabani, Gerald Kakubu, Samweli Kimwiti na Arnold
Kileo huku majengo yaliyokuwa yakitumika kufundishia yakiwa ya chama cha TANU, Mtaa
wa Lumumba.
0 comments:
Post a Comment