Sijawa Omary, Lindi
SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba kufanya ziara ya mafanikio Kusini mwa nchi, CUF mikoa
ya Kusini ya Lindi na Mtwara imetoa tamko la kutomtambua kuwa Mwenyekiti wake halali.
Tamko hilo lilitolewa hivi karibuni na
wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi huo Taifa
na baadhi ya wadhamini wa chama hicho wakati wa mazungumzo na vyombo vya
habari mikoani humo baada ya kumalizika
kwa kikao cha Kamati ya Utendaji ya Kanda kwenye ofisi za chama hicho mjini hapa.
Aidha,
kikao hicho kilishirikisha wajumbe mbalimbali akiwamo mdhamini wa CUF,
Abdallah Khatau kutoka Masasi, Mbunge wa
Tandahimba, Ahmadi Khatani, Mbunge wa Kilwa Kusini Selemani Bungara ‘Bwege’, Mwenyekiti
wa CUF wa Wilaya ya Lindi Mjini, Salum
Bar’wani na viongozi wengine.
Bar’wani wakati akiwasilisha tamko hilo
kwa niaba ya wajumbe wenzake, alitaja
sababu zilizofanya wafikie uamuzi huo kiwa ni kitendo cha kujiondoa kwenye nafasi yake
wakiwa kwenye mapambano ya uchaguzi.
Pia alitaja sababu zingine kuwa ni
kutekeleza na kuheshimu uamuzi halali wa uongozi wa Baraza Kuu la CUF lililokutana
Zanzibar.
Alisema kitendo cha Lipumba kuwaacha
kwenye mazingira magumu ya uchaguzi huku
wanachama na wazee wakimsihi kuacha lakini kuendelea na msimamo wake ni cha
kushangaza hivyo hawako tayari kufanya kazi naye kutokana na udhaifu alioonesha
awali.
Kutokana na hilo, wajumbe hao walikanusha
tamko la baadhi ya watu wanaojiita viongozi na kwamba wanamuunga mkono Profesa.
‘’Baadhi ya watu wamekuwa wakitoa maneno
ya uongo kwa chama cha CUF, sisi viongozi tunapenda kukanusha maneno haya na
hatukubaliani nayo,’’ alisisitiza Bar’wani.
Alisema,
wanaungana na viongozi wenzao kupinga alichokiita msimamo wa ushauri wa
Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Jaji Francis Mutungi kwamba ushauri wa
kumrejesha na kumtambua Lipumba kuwa kiongozi ni kinyume na Katiba ya CUF.
Tamko hilo liliwataka watendaji wa
wilaya wa kanda hiyo kutomuunga mkono Lipumba kwa kuwa si kiongozi anayeitakia
mema CUF huku wakiomba wanachama kuwa na subira wakati viongozi wa kitaifa
wakiendelea kushughulikia mgogoro huo.
0 comments:
Post a Comment