Suleiman Msuya
MHADHIRI Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sheria, Dk Onsmo Kyauke amekosoa kitendo cha
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuegemea upande katika mgogoro
wa kisiasa ndani ya CUF, akidai ni udhalilishaji wa taaluma ya sheria nchini.
Dk Kyauke alisema hayo jana alipozungumza
na JAMBO LEO Dar es Salaam, siku chache baada ya Ofisi ya Msajili kutoa barua
kwa CUF kuruhusu kufungua akaunti kupitia kwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim
Lipumba jambo alilosema ni kinyume na sheria na Katiba ya chama hicho.
Alisema kulingana na hali ya chama hicho,
Msajili alipaswa kuwa mtu wa kati, kwani
kufanya hivyo ni kuongeza mpasuko na kudhalilisha taaluma ya sheria nchini.
“Nadhani Msajili anapaswa kujiuzulu kwani
kimsingi ameonesha udhaifu, ushahidi upo kwenye mgogoro wa CUF kwa kuandika
barua ya ufunguzi wa akaunti kinyume na taratibu,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF,
chombo chenye mamlaka ya kufungua akaunti ni Bodi ya Wadhamini ambapo benki
husika inapaswa kupokea cheti cha usajili na si barua ya Msajili kama
ilivyofanyika katika mchakato wa kufungua akaunti kupitia Lipumba.
Alisema katika mchakato huo baada ya
benki kupokea maombi inapaswa kupeleka taarifa kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi
na Udhamini (RITA) ambao ndio unatoa taarifa kwa benki husika kuhusu wadhamini
na nia ya kufungua akaunti.
Dk Kyauke pia alisema inasikitisha kuona
Lipumba anafanya mikutano ya hadhara mikoani huku kukiwa na katazo la Jeshi la
Polisi bila kuchukuliwa hatua.
0 comments:
Post a Comment