Sharifa Marira
WAKATI viongozi wakuu wa CUF; Profesa Ibrahim Lipumba
(Mwenyekiti) na Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu) wakiendelea kuvutana,
aliyewahi kuwa kigogo wa chama hicho, Hamad Rashid Mohamed (pichani) amesema mgogoro huo
ni matunda ya dhambi ya ubaguzi.
Katika mahojiano maalumu na JAMBO LEO jana, Hamad
ambaye alikuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni katika Bunge la Tisa
alisema wasipoitubu, dhambi hiyo itawamaliza.
Akitumia uzoefu wake ndani ya CUF, Hamad ambaye
alipofukuzwa kwenye chama hicho akaanzisha Chama cha Alliance for Demokratic
Change (ADC), alitaja mambo kadhaa yanayokiharibu chama hicho kama
inavyofafanuliwa kwenye kipengele kifuatacho cha maswali na majibu;
Swali: Unadhani nini kimejificha
nyuma ya mgogoro wa CUF?
Jibu: CUF kimeondoka katika
muundo wa kuwa taasisi na kimekuwa chama kinachoongozwa na mtu mmoja
anayeshirikiana na watu wawili au watatu tu wanaomuunga mkono.
Sasa kama chama hakipo kwenye muundo wa taasisi,
kitakuwa kinaendeshwa kwa matakwa ya mtu mmoja. Lakini ikiwa watu wanaanzisha
chama kinachoamini katika Muungano halafu ndani yake anatokea kiongozi anasema
anataka Serikali ya Mkataba, hapa kuna tatizo.
Ugomvi CUF utaendelea kwa sababu kuna sultani anayetaka
kusikilizwa kila anachotaka kifanyike bila kujali kina manufaa gani kwa chama.
Kwa mfano mimi nilishutumiwa kwamba nimetaka kugombea
ukatibu mkuu ili nimpiku Maalim Seif. Nikaambiwa napelekwa kwenye kamati ya
nidhamu ambayo haipo kikatiba na baadaye nikapelekwa katika Baraza Kuu la
Uongozi na sikupewa hata nafasi ya kujieleza kwa sababu tu mtu fulani ana
wasiwasi na nafasi yake.
Ukishachukua haya yote unakuta ugomvi ndani ya CUF
utaendelea hadi watakapoondoa dhambi hii. Naamini itawaandama (dhambi) kwani
wamedhulumu sana juhudi za watu, rasilimali na muda wa watu ili watu fulani
wabaki kwenye madaraka na kutumia hata uongo ili wabaki katika nafasi zao.
Swali: Kuna sababu nyingine iliyofanya ufukuzwe CUF?
Jibu: Walinizushia nimepewa fedha na Pengo (Kardinali),
Pinda (Waziri mkuu mstaafu) na Lowassa (aliyekuwa mgombea Urais kupitia Ukawa)
ambaye ndiye wamemchukua na kufanya naye siasa kila mahala.
Swali: Unashauri Lipumba na Seif
wafanye nini ili wamalize mgogoro huo?
Jibu: Kama hawataki kukaa na
kuangalia Katiba ya Chama bila kumuangalia mtu usoni wataendelea kuteketea.
Swali: Kwa nini CCM hakuna migogoro
mingi kama wapinzani?
Jibu: CCM wana madhambi yao,
lakini wameweka utaratibu wa kuheshimu chama, lakini CUF inafukuza watu kwa
sababu haiendeshwi kitaasisi.
Swali: Lakini kuna madai kuwa
wewe unatumika na CCM?
Jibu: Sishangai kusikia hivyo,
kwa kuwa hao hao wanaoniambia natumika na CCM walinishutumu natumika na Chadema
nilipokuwa Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni. Nishazoea kushutumiwa
ila tofauti yangu na wao ni kwamba mimi siwezi kutumia lugha ya matusi katika
kuwajibu.
Swali: Kuna watu wanaamini kuwa ni
tabia ya Seif anapomchoka mtu (mwenyekiti) anatengeneza zengwe. Wakitolea mfano
kwa wenyeviti wastaafu kama kina Mapalala. Wewe una maoni gani?
Jibu: Ni kweli kwa mfano Mzee
Mloo alikuja akasema anataka apumzike, lakini baadaye akaona aendelee na akapita
kwa Katibu Mkuu (Seif) na alimkubalia, ila baadaye yakatengenezwa mazingira
kuwa kauli yake aliyoitoa awali ndiyo iwe hiyo hiyo, hakuangalia kwamba ni mtu
ambaye amejitolea katika chama.
Kuna watu walijitoa sana katika chama wakadhalilishwa
na kufukuzwa, sasa hiki kinachotafuna CUF ni matunda ya dhambi ya ubaguzi na ubinafsi.
Swali: Unadhani nani kakosea kati ya
Lipumba na Seif?
Jibu: Naona wote walikosea kwa namna
walivyojiunga na Ukawa. Hawakuangalia madhara yanayoweza kukipata chama.
Walikosea kwa sababu uamuzi ule haukuwa na baraka za
mkutano mkuu wa chama. Ilikuwa ni lazima mkutano wa CUF ukubali kwanza kwamba
hawatasimamisha mgombea Urais kabla ya kujiunga na Ukawa, lakini wao wakajiamlia
kirafiki rafiki.
Chadema walikuwa wajanja walienda katika mkutano wao
mkuu kuomba baraka na wakawazidi ujanja wengine kwa kulazimisha kumpitisha
Lowassa.
Swali: Unadhani ni kwanini Seif na
Lipumba hawakushitukia njama hizo?
Jibu: Msajili alikuwa sahihi kwa
kuwa alizingatia Katiba ya CUF inavyosema. Hakupendelea upande wowote. Ukiisoma
Katiba ya CUF hata wewe ambaye siyo mwanasheria utakuwa upande wa msajili.
Swali: Kwa mgogoro uliopo nini
inaweza kuwa hatima ya CUF?
Jibu: Naona CUF ikimfia Maalim
Seif
Swali: Unaionaje CUF ndani ya
Ukawa?
Jibu: CUF imemezwa na Ukawa.
Haiwezi kuendesha siasa ikiwa ndani ya umoja huo wa vyama vinne.
Swali: Unaweza kutofautishaje
mgogoro wa sasa kati ya Seif na Lipumba na ule kati yako na Seif hata
ukatimuliwa na kuamua kuunda chama kingine?
Jibu: Tofauti yake ni kwamba stori
zetu zilivyotengenezwa tulitakiwa tupate tafsiri ya kisheria zaidi lakini
mgogoro wa sasa unaendeshwa na siasa. Suala letu lilipata Baraka kwa wanachama
wengi wa CUF waliamini tuna makosa hadi sasa ndio wanatufuata kutuomba radhi
tofauti na sasa ambapo watu wengi wa Zanzibar na Bara wanamuunga mkono Lipumba.
Baada ya kushindwa kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Rais Zanzibar kupitia ADC,
Hamad Rashid Mohamed akateuliwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein kuwa mmoja wa mawaziri
katika Serikali yake ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
0 comments:
Post a Comment