Mwandishi Wetu
IKIWA umepita mwezi mmoja na juma moja tangu polisi wapambane na
majambazi kwa zaidi ya saa 6, eneo la Vikindu wilayani Mkuranga, taarifa mpya
zinaeleza kwamba kiongozi wa wahalifu hao wanaodaiwa kuua polisi eneo la Mbande
anayetajwa kuwa ni komando aliwatoroka polisi kupitia juu ya dari.
Taarifa hizo zimekuja siku chache baada ya watu waliokamatwa katika
tukio hilo lililotokea
mkoani Pwani kuruhusiwa
kurejea kwenye nyumba hiyo ya
mapambano, huku wakihakikishiwa
ulinzi.
Habari za kiuchunguzi zinaeleza kuwa wakati polisi walipokuwa
wakiendelea kutupiana risasi na majambazi hao, komandoo huyo aliyekuwa na
wenzake, alitumia mwanya huo kutoboa dari, kasha bati kwa risasi na kupata
upenyo wa kutoroka kupitia paa la nyumba hiyo akiwaacha polisi bila kujua
alivyotoroka.
“Muda polisi wakipiga risasi kushambulia nyumba wakidhani
watafanikiwa kumuangamiza, yeye alitumia muda huo kujibizana nao, huku akitoboa
dari na bati kwa risasi kusaka upenyo wa kujiokoa,” kilieleza chanzo chetu.
Kiliongeza kwamba kutokomea kwa komandoo huyo kunatokana na ukweli
kwamba eneo hilo la Vikindu licha ya kuwa na msitu, lina maingilio ya Bahari ya
Hindi ambayo yanaweza kutumika kwa urahisi na wahalifu kutoroka.
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, maeneo hayo ya bahari yanamwezesha
mtu kujificha na kutumia vyombo vya bahari, au miamba iliyopo baharini kutoroka,
lakini pia kukimbilia kwenye visiwa vidogo vya uvuvi visivyofikiwa kirahisi na
polisi.
Jambazi huyo anayetajwa kuongoza kundi la uhalifu, anaelezwa aliwahi
kuwamo ndani ya jeshi na kupatiwa mafunzo ya ukomandoo katika nchi mbalimbali,
ikiwamo Cuba kabla ya uraia wake kutiliwa shaka na kuondolewa jeshini. Matukio
ya uhalifu anayotajwa kuhusika nayo ni pamoja na udunguaji ambapo wote
waliouawa wamekuwa wakipigwa risasi za kichwa.
Siku ya
tukio
Mapambano hayo ya polisi na majambazi yalitokea Vikindu Agosti 26,
ambako Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Kuzuia Majambazi kutoka Kanda Maalum ya
Dar es Salaam, Thomas Njiku alipoteza maisha baada ya kupigwa risasi ya kichwa
na majambazi hao wanaosadikiwa kuongozwa na komandoo huyo.
Magari ya polisi zaidi ya 16 yakifika eneo la tukio yakiwa na askari
waliokuwa wameshika silaha tayari kwa mapambano. Polisi hao walivamia nyumba
iliyodaiwa kuwa na majambazi hao usiku na kuanza kuifyatulia risasi kwa lengo
la kuwateketeza.
Wakizungumza na JAMBO LEO jijini Dar es Salaam hivi karibuni wakazi
hao walisema operesheni hiyo ilifanyika siku moja baada ya tukio la mauaji ya
askari wane kwa kupigwa risasi kichwani na mtu anayetajwa kuwa ni komandoo. Kwa
mujibu wa wakazi hao operesheni waliodai iliwanyanyasa, iliongozwa na Kamanda
wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Mbagala, mkoani Temeke, Thobias Walelo
aliyekuwa na askari polisi pamoja na mgambo.
Wakazi hao waliozungumza na JAMBIO LEO kwa sharti la kutotajwa
majina yao gazetini wakihofia usalama wa maisha yao walisema siku hiyo polisi
walioongozana na mgambo waliofika eneo hilo wakiwa na magari manne na kuanza
kufyatua mabomu ya machozi, hali iliyofanya washindwe kuwaona.
Mmoja wa wakazi hao alisema baadhi ya wanakijiji walikuwa wamejikusanya
pamoja na walipokutwa na polisi hao na mgambo waliambiwa wakae chini na
kunyosha mikono juu.
“Tuliulizwa kwa nini ninyi mmejenga maeneo yasiyoruhusiwa,
nilikamatwa nikiwa pembeni kidogo na nyumba yangu na wakati wanaingia na
kurusha mabomu ilikuwa ni saa 11 jioni na kashikashi hizo zilidumu hadi saa moja
usiku,” alisema.
Kamanda wa upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Mbagala, Thobias Walelo
alisema hawezi kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa hana mamlaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi huo, Gilles Muloto alisema hana
taarifa za tukio hilo na kwamba ni mara yake ya kwanza kulisikia hivyo hawezi
kulizungumzia na kulitaka gazeti hili lifuatilie tena taarifa hizo kwa kuwa
eneo hilo halimhusu.
0 comments:
Post a Comment