Dotto Mwaibale
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), kimefungua kesi ya kikatiba kuhusu ulinzi wa haki ya kuishi na
urekebishwaji wa sheria ya kanuni ya adhabu juu ya ulazima wa kutolewa adhabu
ya kifo kwa makosa ya uhaini na mauaji.
Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kikitaka
ufafanuzi zaidi juu ya adhabu ya kifo, kikibainisha kuwa adhabu hiyo haimpi
nafasi mtuhumiwa kujirekebisha bali ni kulipiza kisasi.
Kituo hicho kimesema endapo Tanzania
itatekeleza hukumu ya kifo kwa sasa,
inamaanisha watu wapatao 228 na zaidi watapoteza maisha yao huku wengine 244
wakisubiri rufaa zao.
Akizungumza juzi Dar es Salaam, wakati
akitoa tamko la kupinga adhabu ya kifo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba
alisema hadi mwaka jana jumla ya watu
472 walikuwa wamehukumiwa kunyongwa.
Alisema Kituo kinaiomba Serikali
kurekebisha sheria ya kanuni ya adhabu na sheria ya ugaidi yenye kutoa adhabu
ya kifo kwa makosa ya mauaji, uhaini na ugaidi.
Dk Kijo-Bisimba alisema Kituo kina
sababu za kupinga adhabu ya kifo na hakifurahii
watu kuua wengine na ndiyo maana hakipendi pia muuaji auawe.
“Adhabu ya kifo ni vigumu kuhakikisha
kuwa inatekelezwa tu kwa ambao huwezi kuirekebisha, kwani mfumo wa utoaji haki
huwa pia na mianya ya makosa na hivyo maisha ya mtu yanaweza kupotea bure,”
alisema Dk Kijo-Bisimba na kuongeza kuwa hakuna ushahidi kuwa
adhabu hiyo inaweza kuzuia wengine kutenda makosa kama hayo.
Alisema licha ya adhabu hiyo kutotekelezwa nchini kwa takriban miaka
22 sasa, taarifa zinaonesha kuwa watu 72 walishanyongwa.
Hata hivyo, aliiomba Serikali
kutengeneza utaratibu wa kuelimisha jamii juu ya kuheshimu haki za binadamu
hususan za kuishi na kuweka mazingira ya kuiheshimu haki hiyo.
Pia aliomba ibadilishe sheria kwa
kuondoa adhabu ya kifo na kuweka mbadala kwenye makosa ya jinai na kwa wafungwa
waliopo mfano vifungo vya muda mrefu
gerezani.
0 comments:
Post a Comment