MKURUGENZI
Mtendaji wa Kampuni ya Bakhresa Foods, Said Salim Bakhresa, amesema ataongeza
viwanda vingine vya usindikaji matunda nchini ili kuongeza thamani kwa mazao ya
wakulima.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotumwa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana Dar es Salaam kwa
vyombo vya habari, ilisema kauli hiyo
ilitolewa na Mkurugenzi huyo alipokutana
na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kufanya naye mazungumzo ofisini mwake.
Bakhresa
alisema ana mpango wa kujenga kiwanda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa watu
wanapata usumbufu wa kusafirisha matunda hadi Dar es Salaam kuyauza.
“Kuanzia
Oktoba 15, tutaanza kupokea matunda kutoka Kahama na maeneo ya jirani, na kwa
siku tunapata malori zaidi ya 30 na yakimalizika tunaanza kupokea ya mikoa ya Pwani na Kusini,” ilisema taarifa
ikimkariri Bakhresa.
“Tukijenga
kiwanda Kanda ya Ziwa, tutapunguza adha ya wadau kusafirisha matunda kutoka
kule hadi hapa kiwandani na badala yake sisi tutakuwa tunasafirisha juisi isiyochujwa na kuileta
hapa kwa hatua zaidi za usindikaji,” alisema.
Aliongeza
kuwa ana mpango wa kuendeleza usindikaji wa vyakula vya nafaka kwenye mikoa ya
Kusini na kwamba hadi sasa ameajiri wafanyakazi zaidi ya 8,000 wakiwamo
Watanzania 180 kwenye matawi yake nje ya nchi ambapo hulipwa kama wataalamu.
Alisema
hivi sasa Kampuni hiyo imeshafungua matawi mengine Rwanda, Burundi, Msumbiji,
Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Kampuni
ya Bakhresa Foods inatengeneza juisi, soda, maji, biskuti, barafu, ngano,
mahindi, mchele na bidhaa za kuokwa.
Waziri
Mkuu Majaliwa alimweleza Bakhresa kuwa nia ya Serikali ni kushirikiana
na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kwa kuwa imedhamiria kukuza uchumi kupitia
uzalishaji viwandani.
“Serikali
inathamini mchango wa wenye viwanda katika nchi yetu, tunawashukuru ninyi ambao
ni wakongwe kwenye sekta hii, na kwa hiyo tunawaomba msikate tamaa, endeleeni
kufungua viwanda zaidi ili wananchi wapate mahali pa kuuzia mazao au bidhaa
zao,” alisema.
Alimwomba
Bakhresa aangalie maeneo mengine zaidi ya kuwekeza kama vile kwenye sekta za
hoteli na utalii ili kusaidiana na Serikali kukuza uchumi wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment