Enlesy Mbegalo
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemjibu Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, Jaji Francis Mutungi kikisema ofisi yake haina mamlaka ya kisheria
kutoa msimamo na mwongozo wa chama kilichosajiliwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Hamad, majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa iliyoanzishwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa sura 258 haimpi Jaji
Mutungi mamlaka hayo.
Alisema sheria hiyo inampa mamlaka ya kuhifadhi kumbukumbu na taarifa
za vyama vya siasa na siyo kuviamria vyama.
“Baraza Kuu la Uongozi wa CUF linasikitika na upotoshaji wako wa makusudi
ulioufanywa na ofisi yako kuhusu tafsiri ya vifungu vya Sheria ya Vyama Vya Siasa,
Sura ya 258 ulivyovitaja katika ukurasa wa pili wa taarifa yako fupi ili kujipa
mamlaka ya kushughulikia kile ulichokiita mgogoro wa uongozi katika chama chetu,”
alisema.
Alisema hakuna chama cha siasa kitakachofaulu kupewa usajili wa
kudumu hadi kiwe kimewasilishwa majina ya uongozi wa kitaifa na uongozi wa
chama hicho uundwe na wanachama kutoka Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.
Alisema ukisoma vifungu hivyo katika sheria hiyo utabaini kuwa hakuna
uhusiano na kukupa mamlaka au wajibu wa kuchunguza na kujiridhisha kuhusu
usahihi wa mabadiliko katika uongozi wa kitaifa wa chama na ama kutengua au kubariki
uamuzi halali wa vikao halali vya chama chochote.
Aliongeza kuwa kwa kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Lipumba na kutengua
barua yake Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF linatambua kuwa chama cha
hicho kinaongozwa na Katiba yake halali, toleo la mwaka 2014.
“Tunapenda utambue (Msajili) kuwa kujiuzulu kwa kiongozi ni wakati
wowote kwa mujibu wa Ibara ya 117(1). Kuhusu utaratibu uliowekwa na ibara ya
117(2) hauathiri haki ya kiongozi kujiuzulu wakati wowote,” alisema Maalim
Seif. Alisema Profesa Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya Mwenyekiti
wa CUF Taifa kuanzia tarehe 5/08/2015.
Alisema Lipumba alijiuzulu rasmi nafasi yake ya uenyekiti wa Taifa CUF
Agosti 5 mwaka jana huku akidai kuendelea kuwa mwanachama na kadi yake
aliilipia mpaka 2020 hivyo alitekeleza kujiuzulu kwake bila kusubiri kukubaliwa
na Mkutano Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Ibara 117(2) ya Katiba ya CUF.
Aliongeza kuwa Lipumba alikuwa na mamlaka ya kuhakikisha Mkutano
Mkuu unaitishwa ili kukubali kujiuzulu kwake, lakini hakufanya hivyo.
“Kama ulivyoeleza katika taarifa yako, Katiba ya CUF inatambua haki
ya kujiuzulu uongozi lakini haizungumzii kutengua uamuzi wa kujiuzulu,”
alisema. Maalim Seif alisema Profesa Lipumba asingeweza kutengua uamuzi wake wa
kujiuzulu kwa sababu alishautekeleza.
Alisema suala la Profesa Lipumba kurudi kwenye nafasi ya Mwenyekiti
wa CUF Taifa baada ya zaidi ya miezi kumi ni wazo chelewefu na ndiyo maana
amekuwa akiitika wito wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kama mwaliko kutoa
maoni juu ya mambo mbalimbali.
“Tambua pia kuwa Katiba ya CUF ni yetu wenyewe na wewe ni Msajili,
tunaifahamu vyema sisi wanachama na viongozi kuhusu maudhui yake kuliko wewe
ambaye mara zote tunakupa taarifa baada ya maamuzi ya vikao na Katiba hiyo kuwasilishwa
kwako kwa usajili tu,” alisema. Alisema kujiuzulu kwa Lipumba kulifanyiwa
maamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 115(1) ya Katiba ya CUF na siyo ibara ya 77(7).
0 comments:
Post a Comment