Fidelis Butahe
WAJUMBE 47 kati ya 71 wa mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa ya Chama
cha NCCR-Mageuzi juzi usiku walimchagua Danda Juju kuwa Katibu Mkuu mpya wa
chama hicho.
Danda ambaye kwa takribani miaka mitano alikuwa
msaidizi wa mwenyekiti wa chama hicho Taifa, James Mbatia, aliibuka mshindi
katika uchaguzi huo uliofanyika kuziba nafasi tatu zilizokuwa wazi, ikiwemo ya
aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe aliyejiuzulu hivi
karibuni.
Uchaguzi huo uliojaa kila aina ya
mvutano na maneno ya hapa na pale, ulimalizika saa 4:10 usiku, huku aliyekuwa
mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliyejitosa kuwania ukatibu mkuu,
akijitoa dakika za mwisho na kuzua minong’ono miongoni mwa wajumbe.
Kafulila ambaye ameanguka katika kesi ya
kupinga ushindi wa mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini (CCM), Husna Mwilima,
alikuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi ya chama hicho.
Kwa ushindi huo, Danda anakuwa Katibu
Mkuu wa saba wa chama hicho tangu kilipoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 90.
Mbali na Danda, chama hicho pia
kilichagua Naibu Katibu Mkuu Bara na Mweka Hazina.
Akizungumza na JAMBO LEO, Mkuu wa Idara
ya Organaizesheni na Utawala wa chama hicho, Florian Rutayuga alisema: “Wajumbe
wa mkutano wa Halmashauri Kuu wapo 84, lakini waliopiga kura walikuwa 71.
Kafulila alijitoa dakika za mwisho, baada ya kuitwa kuhojiwa kama walivyofanya
wenzake. Baada ya kujitoa Danda alipambana na Faustine Sungura ambaye alipata
kura 24.”
Alisema kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu
Bara, Elizabeth Mhagama aliibuka mshindi, baada ya kupata kura 67 na
kuwashinda, Hassan Mlage (4) na Hassan Luanya ambaye hakupata kura hata moja.
“Kwa mweka hazina, Mike Kalava alishinda
baada ya kupata kura 52 huku Beati Mpitabakana akipata kura 19,” alisema.
Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho,
Danda atalazimika kupendekeza majina ya wakuu tisa wa idara za chama hicho kwa
ajili ya kupitishwa na mkutano wa Halmashauri Kuu Taifa.
Waliowahi kuwa makatibu wakuu wa chama
hicho ni Mabere Marando, Prince Bagenda, Dk Ringo Tenga, Mwaiseje Polisia,
Samwel Ruhuza na Nyambabe.
0 comments:
Post a Comment