Sharifa Marira
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani
Kikwete (CCM) ameiomba jamii hasa vijana, kujenga tabia ya kujitolea damu ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji katika
vituo vya vya afya na hospitali mbalimbali nchini.
Aidha amewahamasisha wananchi kupima
afya zao mara kwa mara kwa lengo la kujua maradhi yanayowakabili na kupatiwa
matibabu mapema kabla ya magonjwa kukua na kuleta madhara.
Ridhiwani aliyasema hayo juzi Chalinze
katika kampeni ya kuchangia damu salama iliyotambuliwa kama " Changia Damu
Salama kwa mama na mtoto", ambapo alikuwa ni mgeni rasmi katika kampeni
hiyo.
Alisema tatizo la damu ni kubwa na kuna
umuhimu wa kuchangia pamoja na kupima afya kila wakati ili kuweza kujikinga ama
kutibu magonjwa mapema kabla ugonjwa haujakua.
“Tujitolee damu ndugu zangu kuwa wenye
mahitaji ni ndugu zetu,'mama zetu, watoto wetu na watanzania wenginw wenye
mahitaji,” alisema.
Aliongeza: “Licha ya kuwa mgeni rasmi,
siwezi kuja kuangalia watu wakichangia damu wakati mimi mwenyewe ninayo damu ya
kutosha kuchangia.”
Alieleza kuwa takwimu zinaonesha kwamba watoto
chini ya umri wa miaka mitano mkoani Pwani wako kwenye hatari ya kupoteza
maisha kutokana na upungufu wa damu na kwamba kwa hali hiyo kuna kila sababu ya
kuokoa maisha ya watoto hao.
Alisema watoto wenye umri huo wamekuwa
wakiongoza kwa kukosa damu kutokana kuugua ugonjwa wa malaria, lakini pia
kutofikishwa hospitali mapema.
Ridhiwani alitaja kundi jingine lililo
hatarini kuwa ni kinamama wajawazito na majeruhi wa ajali aliosema wamekuwa
wakipata tatizo la ukosefu wa damu hasa wanapohitaji kufanyiwa upasuaji.
0 comments:
Post a Comment