Is-haka Omar, Zanzi bar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), hakina mpango wa kufanya mazungumzo au
makubaliano na CUF kuhusu uchaguzi uliopita.
Msimamo huo ulitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai
Ali Vuai wakati akijibu hoja za Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa
Ladhu kwenye mahojiano maalumu na gazeti moja nchini juzi.
Alisema uchaguzi umekwisha, kazi iliyo mbele ni kusimamia
utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/20 ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa
kwenye kampeni za uchaguzi mkuu zinatekelezwa kwa vitendo.
Vuai alisema Jussa alinukuliwa akisema CUF inaangalia uwezekano wa
kufanya mazungumzo na CCM kuhusu uchaguzi, jambo ambalo CCM haiko tayari kukaa
meza moja na chama hicho kujadili jambo ambalo lilishafanyiwa uamuzi halali kwa
mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za nchi.
Alisema chama hicho kinaweza kukaribisha chama chochote cha
upinzani kuzungumzia kuimarisha na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM na si
uchaguzi mkuu ambao ulipita kisheria na serikali zinaendelea kutumikia wananchi
kwa uadilifu.
Alisema kujadili serikali za Zanzibar na Tanzania hivi sasa ni kwenda
kinyume na sheria za nchi kwani zimetokana na uamuzi halali wa wananchi kupitia
uchaguzi wa kidemokrasia.
Alitaka wafuasi wa CCM na wananchi kupuuza madai ya kiongozi huyo
hasa mantiki ya kuundwa kwa Serikali ya Mpito Zanzibar, hatua ambayo alisema
haiwezekani na inaashiria kuvunja Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Pia alisema hoja na ajenda ya kufanyika uchaguzi wa mpito Zanzibar
ni ndoto au kujifurahisha kwa kutafuta umaarufu wa kisiasa usio na uzani wala
mafanikio kwa wafuasi wa chama kinachojenga hoja hizo nchini.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alifafanua kuwa CUF imekosa mwelekeo na
ndiyo maana viongozi wake wanadanganya wafuasi wao kwa mambo ambayo kiuhalisia
wanajua hayawezekani kisiasa Zanzibar.
Alisema jukumu la msingi linalotekelezwa na CCM sasa ni uhakiki wa
mali zake ili kujiridhisha zaidi kama mkakati wa uimarishaji hali ya siasa na
uchumi ndani ya CCM.
0 comments:
Post a Comment