Baltazar Mashaka, Mwanza
MKURUGENZI mstaafu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) Dk. Edward Hoseah ameingia matatani akidaiwa kukwepa kulipa sehemu ya
deni la Sh.milioni 4.5 kwa mkandarasi David Christian, baada ya kukamilisha kazi
ya kukarabati nyumba zake mbili anazodaiwa kumiliki mkoani Mwanza.
Nyumba hizo mbili zinazodaiwa kuwa ziko katika mtaa wa Mkudi, Ghana
katika Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza na zinatajwa kufanyiwa ukarabati na mkandarasi
huyo Aprili 2013, lakini hadi sasa Christian anadai hajalipwa fedha zake Sh, milioni
2.5 licha ya kufuatilia muda mrefu.
Hata hivyo, Dk Huseah mwenyewe jana hakutaka kuzungumza na
mwandishi wa habari hii, akisisitiza mara kadhaa kuwa amestaafu, hivyo aachwe
apumzike. Sehemu ya mazungumzo ya Dk. Hoseah na mwandishi wa habari hizi ni
kama ifuatavyo:
Mwandishi: Samahani, naongea na Dk. Hoseah?
Dk. Hoseah: Yah, ndio mimi naongea. Wewe ni nani na una shida gani?
Mwandishi: Mimi ni mwandishi wa habari.
Dk. Hoseah: Wa chombo gani? Mwandishi: Ni mwandishi wa JAMBO LEO.
Hata hivyo, kabla ya kuulizwa jambo alilotakiwa kutolea ufafanuzi,
Dk Hoseah alisema: “Mimi nimestaafu, kama unataka kuongea na mimi andika
maswali.
Majibizano hayo ya mwandishi na Dk. Hoseah yaliendelea huku
mkurugenzi huyo mstaafu wa Takukuru akishikilia msimamo wake kuwa hana muda wa kuongea.
“Mimi nimeshastaafu na sina muda wa kuongea na wewe tafadhali.
Nakwambia sina muda wa kuongea na wewe,” alisema kisha akakata simu.
Awali, akizungumza na gazeti hili juzi mkandarasi huyo alisema
tangu alipokamilisha kazi hiyo miaka mitatu na miezi miwili amelipwa sehemu ya
fedha za kazi hiyo kinyume cha makubaliano.
Christian alisema baada ya kukamilisha ukarabati, nyumba hizo
zilipangishwa na alipodai malipo akaelekezwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji
la Mwanza, Wilson Kabwe (wakati huo sasa marehemu) amlipe, lakini alipomfuata
aling’aka na kumtaka akamdai mwenye nyumba hizo (Dk.Hoseah).
Alisema kuwa kabla ya ukarabati kuanza alionyeshwa nyumba hizo na
Kamanda Msaidizi wa Takukuru wa Mkoa wa Mwanza wakati huo, Zainabu Bakari baada
ya kutambulishwa kwake na marehemu Kabwe.
“Nilikutana na Zainabu pale Kitwala’s akiwa kwenye gari aina ya RAV
4, alijitambulisha kuwa ni Kamanda Msaidizi wa Takukuru Mwanza na alielekezwa
na Kabwe kuja kuniona baada ya kuombwa Dk. Hoseah amtafutie mkandarasi mzuri na
mwaminifu wa kukarabati nyumba zilizopo Mkudi,” alisema mkandarsi huyo.
Aliongeza kuwa waliongozana na Zainabu kwenda kumwonyesha nyumba hizo
na baada ya kuziona walikubaliana ukarabati huo ufanyike kwa malipo ya sh. milioni
4.5.
“Kwa kuwa alinitajia mtu mwenye heshima, sikudhani atabadilika na
kuwa dhulumati. Hata marehemu Kabwe hakuwa na tabia mbaya na ndiye
aliyemdhamini Dk. Hosea kupitia kwa Zainabu, hata kabla ni yeye aliyenitumia
ujumbe kwamba kuna mtu wa Takukuru nimempa namba yako, atakupigia usihofu.
0 comments:
Post a Comment