SIKU
moja baada kuibuliwa kwa utafiti unaoonesha kuwa katika kila watu wanne duniani
mmoja ana matatizo ya akili, wanasaikolojia nchini wametaja sababu 10 za
ukichaa kwa Watanzania, ikiwamo ya ugumu wa maisha.
Wamesema
utafiti huo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ulioibuliwa juzi na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu unaweza kuwa wa
kweli na kusisitiza kuwa ni suala linaloweza kutokea katika jamii na hivyo halipaswi
kupuuzwa.
Sababu
zingine ni msongo wa mawazo, kushuhudia mauaji ya kutisha, ajali, kuvamiwa,
ubakaji, kurithi kwa wazazi, mazingira, malezi mabaya, kukosa imani ya dini na
mmomonyoko wa maadili.
Katika
maelezo yake, Mwalimu alisema mwaka jana Tanzania ilionesha kuwa na wagonjwa wa
afya ya akili 311,789 kulingana na takwimu za waliokwenda hospitali
kuchunguzwa.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Kitengo cha Saikolojia, Chris Mauki alisema:
“Matatizo ya akili yanachangiwa na mambo mengi na huwa ni tatizo zaidi mijini,
ndiyo maana takwimu za utafiti zinaonesha Dar es Salaam inaongoza ikifuatiwa na
Mwanza.”
Alisema
msongo wa mawazo ni moja kati ya sababu na ambayo inatokana na mtu kusongwa na
matatizo na hivyo kuwa na maswali yasiyo na majibu juu ya hatima ya maisha yake.
“Akili inabeba vitu ambavyo haina uwezo wa kuvimudu
na kufikia ukomo wa uwezo wake,” alisema.
Alisema
watu kuishi kwenye mazingira magumu katika ukuaji wao huku wakishuhudia matukio
hatari kama kuvamiwa, mauaji, ubakaji na ajali, huchangia kwa kiasi kikubwa matatizo
ya akili.
“Pia
ukikuta mtu aliye kwenye umasikini mkubwa tangu akiwa mdogo huku akishuhudia
migogoro isiyokwisha ya wazazi au walezi na na hata anapokua anaendelea kuishi kwenye
umasikini, humfanya akose matumaini, hivyo kupata tatizo hili,” alisema Mauki.
“Mtu
kutokuwa na imani pia ni tatizo kwani mtu akiwa anamtumaini Mungu hujawa na
imani, hivyo anaona hata kama anapitia katika mambo magumu kuna siku atafanikiwa,”
aliongeza.
Dk
Richard Shukia wa UDSM, Idara ya Saikolojia, alisema kisaikolojia hali ya mtu
kuwa kichaa inaweza kutokea katika njia mbili kuu ambazo ni kurithi kwa wazazi
au familia husika na kutokana na mazingira yanayomzunguka mhusika.
Mhadhiri
Mwandamizi huyo alisema wapo watu ambao wamepatwa na kichaa kutokana na kurithi
kwa wazazi, hivyo dhana nzima ya kusimamia utafiti inaweza isiakisi hali
halisi.
Alisema
wapo wengine wanapata kichaa kutokana na mazingira ambayo yamewazunguka, hivyo
moja kwa moja yanaakisi utafiti ukiwamo ya WHO.
“Kichaa
au hali ya utukutu inaweza kuwa ya kurithi au mazingira yanayozunguka mfano
alichofanya ‘Scorpion’ kwa maelezo ambayo yanasemwa ni mazingira,” alisema.
Aidha,
alisema hali hiyo ya ukichaa inaweza kuchangiwa na msongo wa mawazo hali ambayo
inasababisha mhusika kuamini kuwa hana cha kupoteza.
Mhadhiri
Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Elimu Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere (MNMA), Dk Berther Losioki alisema malezi ni sababu ya jamii kuingia
katika hali ya ukichaa.
Alisema
pamoja na utafiti huo wa WHO bado Tanzania inapaswa kufanya utafiti ili kuwa na taarifa
sahihi ya hali ilivyo jambo alilodai kuwa litasaidia kukabiliana na tatizo.
Alisema
familia ambayo imelelewa katika maadili na malezi bora ni ngumu kupatwa na hali
ya ukichaa hivyo kuzitaka familia kuishi maisha yenye misingi sahihi ya
kifamilia.
Mkuu
wa Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Dk Abuu Mvungi alisema hajaona utafiti huo
wa WHO ila kwa upande wa mmomonyoko wa maadili, anaamini asilimia kubwa
unachangiwa na vyombo husika kushindwa kusimamia majukumu yake.
Alisema
jamii inaishi itakavyo na wakati mwingine ikichukua hatua za kutaarifu vyombo
husika hakuna uamuzi ambao yanachukuliwa yenye tija kwao.
“Mfano
ukiangalia historia ya tukio la ‘Scorpion’ unagundua kuwa Jeshi la Polisi
halikufanya kazi yake ipasavyo na kama lingetekeleza tukio kubwa lilotokea awali,
lile lisingetokea. Wapo ambao watafikiria kuwa utafiti wa WHO ni sahihi kumbe
sisi ndio sababu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment