MKUU wa Wilaya
ya Bahi, Elizabeth Kitundu amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuacha kujisaidia
porini, badala yake wajenge vyoo vya kisasa kwa ajili ya kujilinda na magonjwa
ya milipuko.
Kitundu aliitoa
kauli hiyo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Unawaji Mikono Duniani iliyoambatana
na kufikia ubora wa usafi wa mazingira katika Vijiji vya Zanka na Mayamaya wilayani
Bahi.
Miradi hiyo ya usafi
wa mazingira wilayani humo inatekelezwa na Shirika la Plan International chini
ya Mradi wa Usafi wa Mazingira Tanzania (Umata).
Kitundu alisema
katika Wilaya ya Bahi kuna Kata 22 na vijiji 59 na kwamba ni wajibu
wa wenyeviti na watendaji kuhakikisha kaya zilizopo eneo hilo zinaacha
kujisaidia porini na zijenge vyoo vya kisasa.
Alisema kujenga
vyoo vya kisasa pamoja na kunawa mikono anapotoka chooni ni jambo la lazima kwa
wakazi wa wilaya hiyo.
“Tatizo kubwa
lipo katika Kijiji cha Mayamaya, kaya 758 hazina vyoo na 348 zilikuwa na vyoo.
Natoa agizo tujenge vyoo vya kisasa pamoja na kunawa mikono tunapotoka chooni,”
alisema
Naye Kaimu
Mkurugenzi wa Programu ya Umata kutoka Shirika la Plan Internation, Judith
Maire alisema lengo ni kuwa na jamii safi hasa Dodoma iwe katika mazingira
safi na salama.
Judith alisema
programu ya Umata inatekelezwa katika Wilaya za Mkoa wa Dodoma ambazo ni
Bahi, Chamwino na Kongwa, huku uchaguzi wa Wilaya hizo ukizingatia hali hafifu
ya usafi wa mazingira na magonjwa ya milipuko kulinganisha na wilaya zingine.
0 comments:
Post a Comment