MWAKA MMOJA MADARAKANI
Fidelis Butahe
SIKU 20 kabla ya Rais John Magufuli kukamilisha mwaka
mmoja madarakani Novemba tano mwaka huu, kuna mambo manane ambayo yanaweza
kutajwa kuwa ndiyo yaliyotikisa taifa katika utawala wake.
Mambo hayo kati ya mengi, yamelitetemesha Taifa kwa
nyakati tofauti kutokana na kasi ya Rais Magufuli kiutendaji, huku baadhi ya
watu wakifurahia hatua hizo na wengine kuumia na kunung’unika kwa kuguswa katika
maeneo yao ya utendaji.
Baadhi ya mambo hayo ni kufuta safari za nje, kufuta
sherehe za kitaifa, kutangaza Serikali kuhamia Dodoma na kuondoa watumishi hewa
Mambo mengine ni kuzuia mikutano ya siasa, ‘kutumbua’
watendaji wa Serikali na taasisi zake, kuzuia taasisi zake na zile za umma kutumia
kumbi za mahoteli au za kukodi kwa kufanya makongamano na mikutano.
Jambo jingine ni lile la wiki iliyopita alipowataka watendaji wote wa Serikali walioalikwa katika
sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge kutohudhuria hafla hiyo na kurejesha posho
walizopewa.
Waliozuiwa kuhudhuria sherehe hizo ni pamoja na wakuu wa
mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala na wakuu wa idara
mbalimbali.
Wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wametaja baadhi
ya mambo hayo kuwa yamekuwa na tija kwa taifa, lakini wakaponda mengine
wakisema hayakuwa na msingi kufanywa.
Walichosema
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard
Mbunda alisema mambo hayo ni mazuri na kwa sababu rais ana madaraka makubwa, akiyatumia
vyema anaweza kuliletea Taifa maendeleo.
“Sidhani kama marais waliotangulia na hata baadhi ya watu
walitarajia kuona haya anayofanya Magufuli.
Watanzania sasa wanatakiwa kutazama uwezo wa kiongozi kuliko kuvutiwa na
chama,” alisema Mbunda.
Alisema Tanzania ni nchi masikini hasa katika miundombinu
na huduma za jamii, lakini umasikini huo unaweza kuondoka iwapo nchi itapata
viongozi wenye kufikiria maendeleo. Alitolea mfano uthubutu wa Rais kulifufua Shirika la
Ndege Tanzania (ATCL).
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT) Hamad Salim, aliungana
na Mbunda katika hoja ya kutaka nchi kuwa na maendeleo, lakini akasisitiza kuwa
ni lazima iwe na mwongozo utakaofuatwa na viongozi wote.
“Rais anafanya mambo mazuri lakini binafsi naona kuna
tatizo. Mwalimu Nyerere (Julius-Rais wa Awamu ya Kwanza), alianzisha Azimio la
Arusha akitaka nchi iongozwe chini ya mwongozo wa azimio hilo. Rais wetu
(Magufuli), hana mwongozo wowote ndio maana kuna maamuzi yanatolewa tolewa tu.
Watendaji hawajui nini wanapaswa kufanya na kwa wakati gani,” alisema Salim.
Aliongeza: “Nchi yetu ilipopata Uhuru, Nyerere aliona
wazi kuna vitu vinakosekana kwa kuwa kila mtu alifanya mambo ajuavyo. Ndio
maana akaja na Azimio la Arusha. Magufuli amekuwa akizungumza mambo mengi ila
hajatueleza nini kinatuongoza na kuna mambo yanatokea kwa sababu hatuna
mwongozo.”
Akitolea mfano jinsi watendaji wanavyobanwa na kurejesha
fedha licha ya kuwa zimeshaidhinishwa kwa shughuli mbalimbali alisema: “Wizara
ya Fedha inazipeleka hizo fedha kwa wahusika kwa sababu wahusika wanafuata
mwongozo na taratibu za Serikali iliyopita. Magufuli aje na mwongozo wake
ijulikane msimamo na mtazamo wa Serikali yake.”
Alisema wapo baadhi ya watendaji wa Serikali wanaoshindwa
kutoa uamuzi kwa kukosa mwongozo na baadhi kuogopa kuamua jambo kwa kuhofia
kutumbuliwa na mamlaka zao za uteuzi.
Watumishi hewa
Mara baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli
alitangaza kiama kwa watumishi hewa na katika maadhimisho ya Sikukuu ya
Wafanyakazi (Mei-mosi), alibainisha kuwapo kwa watumishi hewa 10,295 serikalini,
kati yao watumishi hao, 8,373 wanatokea Tamisemi
na 1,922 wanatoka Serikali Kuu.
Hivi karibuni katika uzinduzi wa ndege mpya za ATCL, alitaja
tena takwimu hizo.
Kufuta sherehe
Novemba 8 mwaka jana, siku tatu baada ya kuapishwa kuiongoza
Tanzania, Rais Magufuli alitangaza kuokoa Sh225 milioni zilizochangwa
kugharamia hafla ya wabunge na kuagiza zinunulie vitanda kwa ajili ya Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH).
Pia, alifuta Sherehe za Uhuru Desemba 9, mwaka jana na
kuamuru Sh bilioni 4 zilizokuwa zimetengwa zitumike kupanua Barabara ya
Morocco-Mwenge.
Pia aliahirisha sherehe za Muungano, Aprili 26 na kuokoa
Sh bilioni 2 na kutaka zitumike katika upanuzi wa Barabara ya Ghana hadi Uwanja
wa Ndege wa Mwanza.
Kufuta safari za
nje
Novemba 7, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza kufuta
safari za nje ya nchi hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa.
Alisema shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi
zifanywe na kusimamiwa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje na wale
watakaosafiri ni kwa vibali maalum.
Kuhamia Dodoma
Muda mfupi baada ya kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti wa
CCM, Rais Magufuli alitoa kauli ya kutaka Serikali kuhamia Dodoma, huku
akisisitiza atahakikisha Serikali yote inahamia mkoani humo kufikia mwaka 2020.
Kusitisha mikutano
ya siasa
Juni 23 mwaka huu, Rais Magufuli alipiga marufuku vyama
vya siasa kufanya ushindani wa siasa hadi baada ya miaka mitano ili wananchi
wahoji wanasiasa kama wametekeleza yale waliyoyaahidi katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.
Mikutano ya
taasisi za Serikali
Katika hotuba yake bungeni Novemba 20, 2015, Rais
alitangaza hatua kadhaa za kubana matumizi, zikiwemo za warsha, semina,
makongamano na matamasha kufanyika katika kumbi za taasisi za Serikali au
wizara jambo ambalo kwa kiasi fulani lilisababisha hoteli kupoteza wateja wake
wa uhakika, ambao ni taasisi za Serikali.
Kutumbua majipu
Mara baada ya kuapishwa, aliahidi kuwashughulikia
watendaji wazembe ili Serikali yake iondokane na kuwalipa watu mishahara bila
kufanya kazi yoyote.
Uamuzi wake huo umesababisha zaidi ya watumishi 100
kutumbuliwa kutokana na tuhuma mbalimbali, huku baadhi yao wakifikishwa
mahakamani kwa tuhuma mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment