Mwandishi Wetu
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetaka wagombea na vyama
vya siasa vinavyoendelea na kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani
kufanya hivyo kistaarabu kwa kuzingatia Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
NEC imeonya dhidi ya chama au mgombea atakayekiuka
maadili hayo kwamba atachukuliwa hatua bila kusita.
Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar,
Hamid Hamid ametioa onyo hilo, siku chache kabla ya uchaguzi huo Januari 22,
baada ya baadhi ya vyama na wagombea kukiuka maadili na taratibu za kampeni kwa
kutoa matamko yaliyo nje ya sera za vyama vyao.
Alisema kipengele cha 2.1 (m) cha Maadili ya Uchaguzi
kinaeleza Wajibu wa Vyama vya Siasa na Wagombea katika kuendesha shughuli za siasa
wakati wa kampeni, kikivitaka vyama vya siasa, wagombea na wafuasi wao, kukampeni
kwa kuzingatia misingi ya kutangaza sera zisizo za chuki, mifarakano wala
mgawanyiko katika jamii.
“Katika kampeni zinazoendelea, baadhi ya vyama vya siasa
vimeanza kukiuka taratibu za kampeni na maadili na kutumia fursa ya kampeni
vibaya, vinawasema viongozi wa kitaifa, kutoa matamko ambayo kihalisia si ya kunadi
mgombea na kufanya kampeni zisizo za kistaarabu,” alionya Jaji Hamid.
Alisema vyama au wagombea watakaoendelea kukiuka Maadili
ya Uchaguzi katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya
Tanzania na Jimbo la Dimani, Zanzibar watachukuliwa hatua.
Jaji Hamid alieleza kuwa kipengele cha 5.3 cha Maadili ya
Uchaguzi kinaeleza wazi kuwa chama au mgombea atakayekiuka maadili ya uchaguzi
katika jimbo au kata yenye uchaguzi mdogo, atafikishwa katika Kamati ya Maadili
ya ngazi husika na kuchukuliwa hatua stahiki.
Aidha, kipengele cha 5.10 cha Maadili ya Uchaguzi
yaliyokubaliwa na vyama vyote vya siasa, kinafafanua kuwa kamati za maadili ya
uchaguzi Taifa, Jimbo na Kata katika kushughulikia malalamiko na kutoa adhabu,
zinaweza kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kukitaka chama au mgombea
kusahihisha kosa au makosa au kuomba msamaha hadharani.
Hatua nyingine ni kukisimamisha chama au mgombea
kuendelea kufanya kampeni za uchaguzi, kutoza faini, kutangaza jina la chama au
mgombea aliyekiuka maadili kwa kueleza kosa au makosa yake kupitia redio,
televisheni, magazeti na njia nyingine za mawasiliano.
0 comments:
Post a Comment