Mkuu wa Mkoa hana mamlaka kumshusha cheo mwalimu


Abraham Ntambara

Gratian Mukoba
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema kitamburuza mahakamani yeyote atakayetekeleza agizo la mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu la kuwavua vyeo walimu wakuu wa shule 63 mkoani humo kutokana na matokeo mabovu ya wanafunzi, kwani hana mamlaka ya kinidhamu kwa walimu.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Rais wa CWT, Gratian Mukoba, Alisema kuwa kauli hiyo ya Mkuu wa Mkoa ni ya kisiasa na haitekelezeki, kwani kwa mujibu wa sheria, Tume ya Maadili ya Walimu ndiyo yenye wajibu wa kufanya hivyo.

“Mkuu huyo wa Mkoa hana Mamlaka kwa mujibu wa sheria za nchi kwa hiyo anachofanya anakiuka sheria, anavunja sheria. Kwa hiyo sisi tumesikia tamko tunasubiri kuona utkelezwaji wake,” alisema Mukoba.

Aidha, Mukoba alisisitiza kuwa wanaamini kuwa agizo la mkuu huyo wa mkoa haliwezi kutekelezeka kwa kuwa lilitolewa kinyume cha sharia.

Mukoba alieleza kwamba ikiwa litatekelezwa, huyo atakeyekuwa amelitekeleza watamfikisha mahakamani kwani mkuu wa mkoa hana mamlaka ya kumwandikia mtu barua.

Mukoba alisema kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2005 na Sheria ya Utumishi wa Walimu ya mwaka 2005 na kanuni zake za mwaka 2016, mkuu wa mkoa siyo mamlaka ya nidhamu.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi hata Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu, Waziri, Mkuu wa Mkoa, Wilaya ama mtu yeyote hana mamlaka ya nidhamu juu ya mwalimu.

Alibainisha kuwa kabla mkuu wa mkoa kutoa tamko hilo, alitakiwa kufanya utafiti ili kujua sababu za wanafunzi wa Mkoa wa Mtwara kufeli, kwani kuna sababu nyingi zinazoweza kuchangia matokeo mabovu ya wanafunzi.

Alitaja baadhi ya sababu hizo zinazoweza kuchangia matokeo mabovu kuwa ni mazingira magumu ya walimu kufundisha, mila na desturi za jamii ya watu wa Mtwara ambazo bado hazijaipa elimu kipaumbele na hali ya umasikini.

Alisema kuwa hatua za kinidhamu huwa zina utaratibu wake na kufafanua kuwa lazima kuundwe tume ya kufanya uchunguzi pamoja na kumpa nafasi mwalimu husika kujitetea ili kubaini kama  ana kosa ambalo linaweza kufanya aadhibiwe.

Alisema Katiba ya Tanzania inakataza mtu yeyote kuhumumiwa bila kusikilizwa.

Akizungumzia suala hilo, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo alipinga kitendo cha mkuu huyo wa mkoa kuwashusha vyeo walimu kutokana na Shule za Serikali kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani, huku akisema hakuna Sheria yeyote nchini inayompa mamlaka hayo.

“Nashangaa ametoa wapi mamlaka hayo, hata kama angekuwa na mamlaka amejiridhisha kiasi gani kwamba walimu wamechangia wanafunzi kufeli, lakini pia suala la uadilifu wa watumishi hawa linapaswa kuwa chini ya Afisa Elimu sasa ni ajabu kuona RC anaigilia,”

“Kila mtu anafahamu jinsi gani Mtwara hali ya miundombinu ya elimu ilivyo katika mikoa ya pembezoni, shule hazina madarasa ya kutosha, walimu wachache bado wanawacheleweshea mishahara halafu wao bado wanakuwa wahanga wanafunzi wakifeli,” Alisema Suzan.



MWISHO


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo