Hussein Ndubikile
UMOJA wa Wainjilisti Kikristo Tanzania
(Uwakita) umeishauri Serikali kufanya uchunguzi wa uhalali wa matumizi ya nembo
ya halal katika bidhaa za vyakula kama inakidhi matakwa ya Katiba na sheria za
nchi.
Aidha, umoja huo umesema ubora wa bidhaa
za vyakula vya viwandani husimamiwa na Serikali na kuthibitishwa uhalali wa
matumizi yake kwa binadamu na Mamalaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la
Viwango nchini (TBS).
Hatua hiyo imekuja baada ya aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila
mwaka jana, kutangaza kuwa mwaka huu nchi itaanza kunufaika sababu iko mbioni
kuingia kwenye orodha ya nchi ambazo bidhaa zake za chakula zitawekwa nembo
hiyo na kuuzwa katika mataifa 33.
Akizungumza na gazeti hili, Mjumbe wa
umoja huo, Elieza Shinza alisema kitendo cha baraza hilo kusisitiza matumizi ya
nembo hiyo ni kuingilia majukumu mamlaka hizo na kwamba endapo itaruhusiwa
kutumika inaweza kusababisha ubaguzi wa kiimani na kuleta mgawanyiko katika
jamii.
“Kuhusu nembo ya halal mpaka sasa hakuna
ushahidi wa kampuni yoyote iliyokataliwa kuuza bidhaa zake nje sababu ya kukosa
nembo hiyo kwa msingi huo madai ya Bakwata si ya kweli kwani wanajua uhalali wa
mamlaka hizi zote,” alisema.
Alisema endapo Serikali itaruhusu nembo
hiyo itumike itakuwa inakiuka Katiba ya nchi ibara ya 13 ambayo inasisitiza usawa wa watu
wote mbele ya sheria na kukataza ubaguzi wa aina yoyote.
Alisisitiza kuwa ibara hiyo katika
kifungu cha nne inapiga marufuku mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote
inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa
shughuli ya mamlaka ya nchi.
Aliongeza kuwa ni vyema Serikali
ikatupilia mbali matumizi nembo hiyo kwani ikiruhusiwa itakiuka Sheria ya TFDA
na TBS.
0 comments:
Post a Comment