Salha Mohamed
WAKULIMA na wafugaji mkoani Morogoro wamewataka
mawaziri watatu kufika mkoani humo ili kutafuta suluhu ya migogoro yao.
Mawaziri hao ni wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, William Lukuvi, wa Kilimo na Chakula, Charles Tizeba na wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.
Hatua ya wakulima na wafugaji hao
ilifikiwa baada ya kuwa na migogoro yenye madhara kwa kusababisha vifo vya watu
na mifugo na uharibifu wa mazao.
Wakizungumzia changamoto na migogoro
wanayopata wafugaji mkoani humo juzi kupitia Kituo cha Televisheni cha Clouds
katika kipindi cha Clouds 360, walisema chanzo cha migogoro hiyo ni mipaka,
huku Serikali ikishindwa kuwasaidia.
Mmoja wa wafugaji mkoani Morogoro,
Kalaita Motosya alisema migogoro mingi inayotokea mkoani humo husababishwa na
ardhi kutokana na kutokujua mipaka yao.
Motosya ambaye ana ng’ombe 200 alisema
maeneo yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya wafugaji ni machache ikilinganishwa
na idadi ya wafugaji walio kwenye maeneo hayo.
“Maeneo yenye mgogoro Serikali ilivuruga
mpango halali wa vijiji na kudai vipo vilivyoanzishwa vibaya na kudai kutafuta
mwekezaji,” alisema.
Alisema kutokana na wafugaji kutafuta
malisho hasa nyakati za kiangazi, hukimbilia sehemu zenye maji ili kunywesha
mifugo yao ndipo hukutana na wakulima wakiwa maeneo hayo ndipo mgogoro
unapoanza.
Alisema kila binadamu ana asili ya
kibinadamu, hivyo mfugaji anaweza kuingiza mifugo kwenye shamba la mkulima kwa
bahati mbaya au kuzidiwa na idadi ya ng’ombe.
Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa
wakulima mkoani humo, Bakari Shafii alisema wafugaji wamekuwa wakiingiza
ng’ombe kwenye mashamba yao kwa makusudi na pindi wanapobaini huambiwa waachwe
ng’ombe wale.
“Ukikuta ng’ombe shambani, ukimfuata
mfugaji na kushauriana kuwatoa labda wamemshinda, hukwambia waache kwani mazao
yana gharama gani,” alisema.
Alisema inapofikia hatua hiyo, mkulima
anapobaini kupata shida wakati akilima ndipo suala la kushambulia mifugo hujitokeza
baada ya wafugaji kukaidi kutoa ng’ombe mashambani.
Alisema wamechoka kuuawa na wafugaji,
kwani wengi wamekuwa wakichukua sheria mkononi huku wafugaji wakiwadharau.
Kutokana na hali hiyo, Shafii alitaka mawaziri
hao kukutana ili kupata suluhu ya mgogoro ambao unahatarisha maisha yao.
Motosya aliitaka Serikali pia kuboresha
miundombinu ya wafugaji kama kutengeneza vyanzo vya maji na maeneo ya malisho
ili wafuge kisasa.
0 comments:
Post a Comment