*Yapongeza ukuaji uchumi, ukusanyaji mapato, vita dhidi ya rushwa
*Yataka sekta
binafsi ishirikishwe utekelezaji wa sera za Serikali
Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
SHIRIKA la Fedha
la Kimataifa (IMF), limeitaka Serikali ya Tanzania, kulegeza masharti ya
mzunguko wa fedha kwa kuuongeza kupitia kuimarisha sekta binafsi, ili kujenga
msingi wa uhakika wa kuendelea kukua kwa uchumi wa nchi.
Taarifa ya Ofisa
Habari kutoka Idara ya Mawasiliano ya IMF, Andrew Kanyegirire, iliyowekwa kwenye mtandao
wa Shirika hilo jana, ilieleza kuwa tamko hilo lilitolewa baada ya kukamilika
kwa kikao cha Bodi ya Utendaji ya Shirika hilo, kilichofanya mapitio ya tano ya
uchumi wa Tanzania.
Tamko hilo la
IMF, linaipongeza Serikali kwa kuimarisha uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei,
kupunguza pengo linalotokana na ununuzi nje ya nchi, ikilinganishwa na mauzo ya nje na
kufikia vigezo vya malengo ya kiuchumi kupitia utekelezaji wa sera zake.
Hata hivyo, IMF
ilionya kuwa ukuaji mzuri wa uchumi ulioonekana katika nusu ya kwanza ya mwaka jana,
uko hatarini kuwa endelevu kutokana na ubanaji wa mzunguko wa fedha.
Pongezi
IMF ilisema
uchumi mpana wa Tanzania uliendelea kuimarika na ukuaji wake kuwa katika
viwango vinavyoridhisha katika nusu ya kwanza ya mwaka jana na unatarajiwa kukua
kwa asilimia saba kwa sehemu iliyobaki ya mwaka.
Shirika hilo
lilipongeza kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei, uliofikia chini ya malengo ya asilimia
tano na vipimo vikionesha kuwa mfumuko huo utaendelea kuwa katika kiwango kinachoridhisha
katika nusu ya mwaka iliyobaki.
Pia liliridhishwa
na namna pengo linalotokana na matumizi ya fedha za kigeni katika ununuzi wa
mahitaji ya Taifa kutoka nje ya nchi, ikilinganishwa na mauzo ya Taifa katika
soko la kimataifa, lilivyopunguzwa kutokana na kupungua kwa ununuzi wa huduma
na bidhaa za nje ya nchi.
Shirika hilo pia
lilieleza kuwa pamoja na utekelezaji wa baadhi ya sera kuwa wa kusuasua, lakini
Serikali hivi karibuni ilifanyika kazi utekelezaji wa baadhi ya sera, zikiwamo
hatua zilizochukuliwa katika makusanyo wa fedha za umma, kudhibiti deni la
Taifa, kuboresha mfumo wa sera ya fedha na kuboreshwa kwa usimamizi wa
mashirika ya umma.
Pongezi zingine zilielekezwa
kwenye utekelezaji wa ajenda ya mabadiliko katika uchumi kama ilivyoelezwa
katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na mapambano dhidi ya rushwa na
kuzuia uvujaji wa mapato ya kodi, ambavyo viliongeza mapato ya Serikali.
IMF ilieleza
kuwa kama mapambano hayo yatakuwa endelevu, Taifa litakuwa limejijengea
matarajio ya uwekezaji mkubwa katika miundombinu kuanzia utekelezaji wa Bajeti
ya 2016/17.
Shirika hilo pia
lilielezea mafanikio ya aina yake katika kubana matumizi, yaliyofikisha
Serikali kupata bakaa ya fedha kati ya Julai na Septemba, baada ya kukusanya
mapato na kudhibiti matumizi, kuwa itasaidia kuwekeza kwenye miradi ya umma na
kuvutia mitaji kutoka nje ya nchi.
Pia lilipongeza
ongezeko la mapato ya fedha za kigeni lililoonekana tangu mwanzo wa mwaka wa
fedha ulioanza Julai mwaka jana.
Hadhari
Pamoja na
mafanikio hayo, IMF ilionya kuwa Taifa linakabiliwa na hatari itakayozuia
kuendelea kukua kwa uchumi kutoka sekta binafsi.
“Kuna hatari
ambayo inaweza kuathiri ukuaji wa uchumi kusonga mbele, inayotokana na masharti
magumu ya mzunguko wa fedha, ukuaji unaosuasua wa utoaji mikopo unaoonekana
kuwa endelevu, utekelezaji unaosuasua wa miradi ya maendeleo na mtazamo wa
sekta binafsi wa kutojiamini kuhusu mikakati mipya ya kiuchumi ya Serikali,”
ilieleza taarifa hiyo.
Kutokana na hatari
hiyo, IMF ilishauri masharti magumu ya mzunguko wa fedha yaliyopo yalegezwe
kupitia sera za fedha za muda mfupi, zitakazotekelezwa kwa nia ya kutimiza
malengo ya kiuchumi.
IMF ilitaka
ulegezaji huo wa masharti ya mzunguko wa fedha, uendane na msukumo wa kuongeza
mikopo kwa sekta binafsi na kushauri Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ichukue hatua
hizo wakati Serikali nayo ikianza kuwekeza kwenye miradi ya umma.
“Kuhusishwa kwa
ukamilifu wake kwa wadau wote katika uundaji na utekelezaji wa sera, ikiwemo
umuhimu wake sekta binafsi, ni muhimu,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Umuhimu wa ushauri
Kikao hicho cha
mapitio ya uchumi, ni sehemu ya Mfumo wa
Kusaidia Utekelezaji Sera (PSI) chini ya IMF ambao taarifa zake hutumiwa na
wabia wa maendeleo, nchi wahisani, benki za kimataifa za maendeleo na masoko ya
mitaji inayoshiriki maendeleo ya nchi husika.
0 comments:
Post a Comment