Jemah Makamba
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imewahukumu
kwenda jela maisha mara mbili na miaka mingine 30 Jackson Simon, Kalambo Matiku
na Marwa Mwita wote wakazi wa Kipunguni, Dar es Salaam kwa ujambazi, kujeruhi
na kunajisi watoto.
Hukumu hiyo ilisomwa jana mbele ya Hakimu
Juma Hassan ambaye alisema katika ushahidi uliotolewa na shahidi wa kwanza
ambaye ni mtoto wa mlalamikaji, ilidaiwa kuwa siku ya tukio Julai 27 mwaka juzi
wakiwa nyumbani Kipunguni wamelala, saa nane usiku walishitushwa na kelele za
baba yao akiomba msaada.
Baada ya hapo walisikia kitu kikimpiga
baba yao na kushuhudia washitakiwa hao wakiingia chumbani mwao na kutokana na
mwanga wa taa waliwatambua ndipo akasikia mmoja akisema: “Haiwezekani yule dereva
bodaboda atudanganye, mbona hatuoni pesa?”
Kisha waliwatolea kisu watoto hao ambao
mmoja alikuwa na miaka 12 na mwingine 15 na kuwalawiti kwa zamu.
Washitakiwa baada ya hapo walichukua
televisheni, mabegi mawili ya shule na simu mbili na kuondoka, watoto walipoingia
chumbani walimkuta baba yao amefungwa kamba.
Walikwenda kuamsha majirani ambao walikwenda
kuripoti kituo cha Polisi cha jirani na kesho yake kuhamia kituo cha Sitakishari na
msako wa kuwatafuta ukaanza.
Kwa kuwa washitakiwa waliiba simu polisi
walifanya utafiti kupitia kampuni moja ya simu na kugundua mmoja kati ya washitakiwa
alikuwa akitumia simu hiyo na kumkamata baada ya kumtegea mtego.
Baba aliyefanyiwa tukio hilo alidai
kupigwa nondo kichwani na kuchomwa kisu na kisha kufungwa kamba kabla
washitakiwa hao hawajahamia kwenye chumba cha watoto.
Shahidi mwingine ambaye ni mtoto aliyelawitiwa
ushahidi wake ulifanana na shahidi wa kwanza ambaye ni dada yake.
Daktari wa Hospitali ya Amana alifika mahakamani
hapo na kuambatanisha fomu za uchunguzi (PF3) ambayo ilionesha watoto hao
kunajisiwa na kulawitiowa na baba kujeruhiwa.
Washitakiwa walikutwa na kesi ya kujibu
na katika utetezi wao, mshitakiwa wa tatu alikataa kujitetea na kunyamaza kimya
huku wengine wakisema hawajahusika.
Hakimu alimuuliza mwendesha mashitaka,
Grace Mwanga kama kuna kumbukumbu za nyuma za makosa ya washitakiwa akasema
hakuna ila wanastahili adhabu kali ili kuwa fundisho kwao kutokana na kitendo
walichofanya.
Hakimu aliwauliza kama wana cha kuimbia
Mahakama kabla hajawapa adhabu, wa kwanza aliomba kuachwa, wa pili akisema atakata
rufaa na mwingine akakaa kimya.
Hakimu alisema kutokana na makosa yao
matatu waliyofanya, la kwanza ni jela miaka 30, la pili na la tatu jela maisha
kila moja.
0 comments:
Post a Comment