Mwandishi Wetu
Balozi Ombeni Sefue |
ALIYEKUWA Katibu Mkuu Kiongozi na
Mwanadiplomasia, Balozi Ombeni Sefue, ameteuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza
kuingia katika Jopo la Watu Mashuhuri katika Mpango wa Afrika Kujitathmini
Kiutawala Bora (APRM).
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM,
tawi la Tanzania Rehema Twalib anayehudhuria Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU)
unaendelea mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, Balozi Sefue aliidhinishwa na
kikao cha juu cha viongozi wa umoja huo.
Alisema nafasi hiyo ya kuwa katika jopo
la APRM haikuwa rahisi kutokana na nchi nyingi kuwasilisha majina ya watu
mashuhuri.
“Balozi Sefue amefanikiwa kuingia katika
jopo hilo la watu mashuhuri, ila naamini inaweza kuchangiwa na utumishi
uliotukuka na kuungwa mkono na Serikali ya Awamu ya Tano,” alisema.
Twalib alisema APRM ni mpango wa Afrika
uliobuniwa na wakuu wa nchi kwa lengo la kuwa na chombo kitakachosaidia
kuhimiza nchi wanachama kuenzi utawala bora na utoaji wa huduma bora za
kiuchumi, kibiashara na za kijamii kwa wananchi wao kupitia mfumo wa
kujitathmini zenyewe na kukosoana.
Katibu Mtendaji huyo alisema kuwa APRM
ni chombo cha juu cha kuwashauri wakuu wa AU katika uendeshaji wa mpango huo na
hususani mchakato mzima wa kujitathmini.
Alisema wajumbe hao wa APRM wanahitajika
kudumu kwa muda wa miaka minne hiyo ikiwa ni baada ya mchakato mrefu kufanyika
ikiwa ni pamoja na ushindani wa wahusika.
Katibu huyo alisema Tanzania ni miongoni
mwa nchi 35 wanachama wa UA kati ya nchi 54 zilizojiunga na APRM. Ilijiunga mwaka
2004 na kwa sasa inaendelea kuteleleza mapendekezo ya mpango huo.
Twalib aliwataja wajumbe wengine walioteuliwa
kuwa ni Profesa Ibrahim Gambari kutoka Nigeria, Balozi Mona Attia Misri, Fatma
Kadaria Algeria, Askofu Don Sengulane Msumbiji na Profesa Augustin Loada
Burkina Faso.
Aidha, alisema wajumbe wa zamani
wanaondelea ni Profesa Youssouf Khalal (Chad), ambaye atakuwa mwenyekiti wa
jopo na Brigitte Mabandla Afrika Kusini ambaye ni Makamu Mwenyekiti.
Alisema pamoja na kuchaguliwa kwa
wajumbe hao pia mkutano huo ulijadili ripoti za tathmini za nchi katika maeneo
ya anuai ya utawala bora kwa nchi za Kenya, Sudani, Chad, Senegali, Djibouti na
Zambia.
Mwenyekiti wa AU ambaye pia ni Rais wa
Kenya Uhuru Kenyatta aliwapongeza wajumbe hao na kuwataka kushiriki vyema
katika kuihuisha APRM na kuwa chombo chenye thamani kubwa kwa Afrika kama
walivyotarajia waasisi wake.
0 comments:
Post a Comment