WASHINGTON, DC, Marekani
DONALD Trump ameapishwa kuwa Rais wa 45 wa Marekani, na
kurudia ahadi yake ya kuifanya nchi yake kuwa taifa lenye nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa
awali.
Hata hivyo, Trump ameapishwa wakati ambao nchi hiyo imegawanyika,
ambapo jana maelfu ya wananchi waliandamana kupinga kuapishwa kwake. Kwa mujibu
wa uchunguzi wa maoni, ni asilimia 40 ya Wamarekani ndio wanamuunga mkono.
Trump aliapishwa huku idadi ya wageni walioalikwa
kuhudhuria sherehe hizo ikiwa ni nusu ya wale waliohudhuria wakati Rais
aliyemaliza muda wake jana, Barack Obama alipoapishwa kwa mara ya kwanza mwaka
2009.
Takribani watu milioni 1.8 walihudhuria sherehe za
kuapishwa kwa Obama wakiwamo watu maarufu na wanamuziki, lakini mambo yashindwa
kwenda sawa kwa Trump kutokana na sherehe zake kuhudhuriwa na wageni takribani 800,000.
Jana Polisi walipambana na kundi kubwa la wananchi waliokuwa
wakiandamana na kuziba mitaa na barabara za majimbo mbalimbali nchini humo wakipinga
kuapishwa kwa Trump kuwa rais wa nchi hiyo.
Trump ambaye alimshinda mpinzani wake wa Chama cha
Democratic, Hillary Clinton katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 8 mwaka
jana, amekuwa akipingwa na kundi kubwa la raia wa nchi hiyo ambao wanasema hakuwa
chaguo lao bali alishinda kutokana na mfumo mbovu wa upigaji kura unaotumiwa na
Taifa hilo.
“Tutaandamana tu wala hatutaogopa kama Polisi watatupiga
au kutukamata, lengo ni kumwonesha Trump kwamba hakubaliki miongoni mwa raia
wengi wa Marekani, haijalishi ameshinda na anaapishwa, katu hatopata nafasi nyoyoni
mwetu.
“Hajawahi kuwa na sera zinazoonesha kama ni kiongozi wa
kutazamwa, kauli zake za kibaguzi kuanzia rangi na wanawake vinamfanya kuwa
Rais wa ajabu kuwahi kutokea Marekani,” alisema mmoja wa waandamanaji katika
eneo la San Diego, California.
Democrats
Sherehe hiyo iligubikwa na mabadiliko mengi mahsusi
tofauti na ilivyozoeleka kwa watangulizi wake.
Jambo kubwa mbali na maandamano hayo yaliyoendeshwa na
wafuasi wa chama cha Democrats, ni uchaguzi wa Trump wa Biblia ambayo alitumia
kuapia, kwani alichagua aliyotumia utotoni, lakini pia kiutaratibu alitumia
Biblia ya Lincoln ambayo ilitumiwa katika viapo vitatu vilivyotangulia.
Biblia hiyo ilitumiwa na Abraham Lincoln mwaka 1861 na
Barack Obama mwaka 2009 na mwaka 2013.
Tofauti na viapo vya nyuma, idadi ya waburudishaji
haikuwekwa wazi kutokana na wengi waliokuwa wamejulishwa kushiriki walijijitoa
kutokana na upinzani wa kisiasa uliogubika sherehe hizo.
Mmoja wa waburudishaji waliothibitishwa tangu awali ni
Jackie Evanco (16) ambaye ni maarufu kwa albamu yake ya ‘America’s Got Talent’
na ndiye aliyeimba Wimbo wa Taifa.
Jambo lingine lisilo la kawaida ni idadi kubwa ya wajumbe
wa Baraza la Congress wa Democrats ambao walitangaza kususa hafla hiyo, huku
idadi ikionesha kuwa theluthi tatu ya wajumbe wote wa Baraza hilo kutoka
Democrats hawakushiriki.
Hata hivyo ratiba ya matukio ya jana haikutofautiana sana
na ilivyozoeleka katika viapo vilivyotangulia vya marais, hata hivyo, Trump
ambaye alilala na familia yake kwenye jengo la Blair House mkabala na Ikulu ya
White House, alianzia kanisani asubuhi.
Baadaye akifuatana na mkewe, Melania, walikwenda White
House kufungua kinywa pamoja na familia ya Rais Barack Obama kabla ya kwenda
Capitol.
Baada ya kiapo, Obama aliondoka na kumwacha Trump akipata
chakula cha mchana kabla ya matukio mengine kama vile gwaride na shamrashamra
zingine ili kuhitimisha siku hiyo.
Wapinzani
Wapinzani wa Trump usiku wa kuamkia jana walipambana na
polisi na kunyunyiziwa pilipili jijini hapa.
Kundi kubwa la waandamanaji wanaompinga Rais Trump
lilikusanyika mapema nje ya Klabu ya Taifa ya Waandishi wa Habari, ambako
kulikuwa na sherehe zijulikanazo kama ‘DeploraBall’ – tukio ambalo liliandaliwa
na wafuasi wa Trump juzi usiku.
Mamia ya waandamanaji hao waliingia mitaani nje ya klabu
hiyo, wengi wakiimba huku wakibeba mabango ya kumkataa Trump.
Mmoja wa wafuasi wa Trump ambaye alikuwa eneo hilo lakini
hakuhudhuria hafla hiyo, alidai kuwa waandamanaji hao walifanya vurugu –
wakimshutumu mmoja wao kwa kumshambulia kwa mlingoti wa bendera.
“Nilikuwa nimevalia kofia yangu yenye maandishi ya
‘Ifanye Marekani Taifa Kubwa tena’, na mwanamume mweupe akanifuata kwa nyuma na
kunisukasuka kwa mlingoti wa bendera – nikapoteza fahamu kama dakika moja hivi,”
Jones Allsup (21) aliiambia Fox News.
Wafuasi
Kambi ya Trump kwenye ghasia hizo nayo iliwakilishwa na
waendesha mapikipiki waliotoka sehemu mbalimbali za nchi kuja hapa siku kadhaa
kabla ya jana ambao walijiandaa kukabiliana na waandamanaji hao.
Kundi hilo linalojiita Bikers For Trump liliomba kibali
cha watu 5,000 kukaa kwenye bustani ya John Marshall, huku wakipanga kufanya
mkutano usio rasmi kati ya tukio la kula kiapo na kuanza kwa gwaride.
Muasisi wa kundi hilo, Chris Cox (48), aliiambia Fox
& Friends: “Kwenye tukio hili ambalo tunahitajika, tutajenga ukuta wa
nyama. Tutakuwa bega kwa bega na ndugu zetu na tutakuwa kidole kwa kidole na
yeyote atakayethubutu kuvuka vizuizi vya Polisi,” alionya Cox.
Kabla ya kuapishwa Trump na Makamu wake, Mike Pence na
familia zao walihudhuria ibada kwenye Kanisa la Mt John baadaye wakaenda Ikulu
ya White House kufungua kinywa na familia ya Rais Barack Obama kabla ya
kuelekea jengo la Capitol, kuapishwa na Jaji Mkuu, John Roberts Jr na
kuhudhuriwa na wabunge wa Baraza la Congress.
0 comments:
Post a Comment