Makunga awafunda wahitimu TSJ


Peter Akaro

Mwenyekiti TEF, Theophil Makunga
WAANDISHI wachanga wanaoingia katika tasnia ya habari, wameaswa kuwa wavumilivu na wabunifu kwa sababu ukuaji wa teknolojia umeleta changamoto kubwa katika upashanaji habari.

Hayo yalibainshwa juzi Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Theophil Makunga, wakati akikabidhi vyeti kwa wahitimu 200 wa Kozi ya Uandishi wa habari katika Chuo cha TSJ.

Akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla hiyo, Makunga alisema uhalisia wa tasnia ya habari ni kwamba mwandishi huweza huchukua muda mrefu hadi kufikia malengo yake.

Makunga aliwaeleza wahitimu kuwa wengi itawachukua muda kwenda kuajiriwa, lakini hilo lisiwakatishe tamaa. Wanapaswa kusimamia kwenye ukweli siku zote.

“Nimekuwa mhariri kwa muda mrefu, ukiangalia maisha yangu nilipitia changamoto nyingi. Lakini nilikuwa nasimamia kwenye ukweli. Chombo chochote cha habari kikisimamia ukweli hata kama unaumiza au kufurahisha, kitakuwa kwenye ushindani na watu watakipenda.

“Muwe wavumilivu katika tasnia, changamoto nyingi ni za kawaida, unapokuwa kwenye chombo cha habari watu wengi wanakutazama wewe na kama kazi yako utaifanya kwa kufuata ulichofundishwa utafanikiwa,” alisema.

Alisema wahitimu bado wana safari refu, kuhitimu ngazi ya cheti na stashahada ni hatua ya kwanza, hatua ya pili ni kutumia yale maarifa uliyoyapatiwa ili waonekane kuwa ni waandishi wazuri na baadaye maisha yao kuwa mazuri.

Makunga alisema waandishi wa habari wachanga, wanaingia katika tasnia kukiwa na changamoto kubwa ya ukuaji wa teknolojia, kitu kinachotoa fursa kwa kila mtu kuripoti habari hata kama hana taaluma hiyo, hivyo mazingira hayo yanawalazimisha kuwa wabunifu.

“Hali ya upashanaji habari umebadilika sana, vyombo vya habari vimekuwa vinazidiwa na mitandao ya kijamii, ingawaje taarifa zake unakuwa huna uhakika nazo.

“Kwa hiyo kesho yake magazeti yanakuja kudhibitisha kile ambacho watu wanakuwa wamekisoma katika mtandao,” alisema Makunga.

Aliongeza licha ya hiyo uandishi wa mtandaoni utachukua muda kwa Tanzania kuwafikia watu wengi na kukubalika kwa sababu ya mazingira yetu, hivyo waandishi bado wana nafasi ya kufanya kazi katika vyombo vya habari vya kawaida.

“Kwa mfano ukienda vijijini hamna umeme, kwa hiyo vyombo vya habari bado vitakuwepo vikiendelea na kazi yake,” alisema Makunga.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo