Celina Mathew
Zitto Kabwe |
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga
limemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ajitokeze kuchukua gari lake
namba T 360 DDV aina ya Toyota Land Cruiser alilolitelekeza uwanjani kwenye
mkutano ingawa kuna taarifa kuwa halimiliki kihalali.
Aidha, Jeshi hilo linaendelea kuchunguza
kuhusu mmiliki halali wa gari hilo kutokana na taarifa za kiintelijensia kuonesha
kuwa Zitto si mmiliki halali na kujitokeza kwa Jaji ambaye hakutajwa jina, aliyedai
kumuuzia gari hilo ila hawakukamilisha nyaraka za
mauziano.
Akizungumza na JAMBO LEO jana, Kaimu
Kamanda wa Mkoa huo, Elias Mwita alisema Zitto anatakiwa akachukue gari lake na
si kama ilivyodaiwa na watu kuwa anatafutwa na Polisi kutokana na uchochezi wa
kisiasa.
"Tunamtafuta Zitto ili aje kuchukua
gari lake aliloacha hapa wakati wa kampeni ambalo kwa sasa tunaendelea
kulichunguza kutokana na kutojulikana mmiliki halali na kwa kuwa Zitto hajaleta
vielelezo, hivyo ni vema akavileta ili tujue kama ni lake au la," alisema.
Aliongeza kuwa ni vema akajitokeza ili
kurahisisha uchunguzi unaofanywa kuhusu gari hilo ambalo halijulikani mmiliki wake
kutokana na kukosekana vielelezo vya umiliki.
Polisi Kahama ambao walichukua gari hilo
lililotelekezwa kwenye kampeni walisema baadaye dereva wa Zitto alipoulizwa
kama vielelezo vipo alijibu havipo.
"Walilichotaka polisi ni kuletewa
vielelezo halali, kwa kuwa siku tulipokuwa tunamtafuta aliliacha uwanjani pale
hadi lilipochukuliwa na polisi kwenda kuhifadhiwa hadi mmiliki halali ajitokeze
na vielelezo," alisema.
Aidha, Kaimu Kamanda huyo aliliambia
gazeti hili jana mchana Zitto aliwasiliana na Jeshi hilo na kukubaliana kuwa atapeleka
vielelezo hivyo ili akabidhiwe gari lake.
0 comments:
Post a Comment