Charles James
Rais John Magufuli |
WASTAAFU wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya zamani
wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati malalamiko yao ya madai ya
pensheni ambayo wamekuwa wakiidai Serikali tangu kuvunjika kwa Jumuiya hiyo
Juni 30, 1977.
Mkataba wa kuvunjika kwa Jumuiya hiyo uliosainiwa mwaka
1984 na marais wa Jumuiya hiyo, Julius Nyerere wa Tanzania, Milton Obote wa
Uganda na Daniel arap Moi wa Kenya, uliagiza kulipwa kwa wastaafu hao na
watumishi waliokuwa wamesitishiwa ajira zao.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na JAMBO LEO,
Mwenyekiti wa wastaafu hao, Mohamed Ngunde ambaye alikuwa mtumishi wa Shirika
la Posta na Simu, alisema kwa kipindi kirefu wamefuatilia malipo yao Hazina,
lakini hakuna hatua ambayo imechukuliwa zaidi ya kuendelea kupigwa danadana.
Alisema wamekuwa wakifuatilia mafao yao katika awamu zote
za uongozi ambapo Novemba 11, 1991 aliyekuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu,
John Malecela aliwaandikia barua kuwataka kuacha kusumbuka, kwani hakuna
wanachodai na hawatalipwa.
Ngunde alisema barua ya Malecela iliwashangaza, lakini
waliendelea kudai haki yao na mwaka 1999, walionana na aliyekuwa Waziri wa
Fedha wakati Jumuiya hiyo ikivunjika, Cleopa Msuya ambaye alikiri kuwa Serikali
ilipaswa kuwalipa kama mkataba wa kuvunjika kwa Jumuiya hiyo ulivyoagiza.
“Baada ya kuonana na Msuya Serikali ilianza kutulipa,
ingawa malipo hayakuwa ya kuridhisha kwani wapo watumishi waliotoka mikoani
lakini waliishia kulipwa Sh 10, Sh 30 hadi Sh 150.
“Mwaka 2003 tulifungua kesi ya kudai mafao yetu, lakini
Serikali ikamwomba Jaji Kimaro aliyekuwa Mahakama Kuu kufuta kesi hiyo ili
wakafanye suluhu, jambo ambalo kwa mujibu wa Mkataba halikuwa sahihi, kwani
hakukutakiwa mazungumzo tena zaidi ya kulipwa stahiki zao,” alisema Ngunde.
Katika hotuba yake Mei mosi, 2005 Rais Benjamin Mkapa
alikiri kufahamu Mkataba huo na kuahidi kuwalipa wastaafu hao zaidi ya Sh bilioni
400 ingawa kidogo kidogo.
“Kila mmoja anajua namna gani nimekuwa nikiheshimu wazee,
hivyo nawaahidi kuwa nitahakikisha kabla sijaondoka madarakani watumishi wote wa
iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaodai mafao yao wanalipwa,” ilisema
sehemu ya hotuba ya Mkapa.
Katibu wa Wastaafu hao, Hamad Wenge ambaye ni mrithi
kutokana na baba yake kutumikia Shirika la Reli, alimwomba Rais Magufuli
kuingilia kati madai yao, ili walipwe kama wenzao wa Kenya na Uganda.
Alisema baada ya tamko la Mkapa walianza kulipwa ingawa
walipewa Sh milioni 2 pekee ambazo zilikuwa za nauli na kibaya zaidi watumishi
waliolipwa walikuwa ni 31,444 badala ya 17,500 waliokuwa halali.
“Tunamwomba Rais Magufuli aingilie kati, kwani tumekuwa
tukimwandikia barua atusaidie au akutane nasi, lakini zimekuwa hazijibiwi jambo
ambalo linaonesha kwamba wasaidizi wake hawamfikishii na mara ya mwisho
tulimwandikia Aprili 4 mwaka jana.
“Tunajua Rais amekuwa akijali maslahi ya masikini na hata
kwenye barua zetu tulirejea kauli zake wakati wa kampeni ambapo aliahidi kama
angeshinda angehakikisha masikini wanaishi kama malaika,” alisema Wenge.
0 comments:
Post a Comment