Charles James
David Kafulila |
WAKATI Mbunge wa zamani wa Kigoma
Kusini, David Kafulila, akiiponda ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),
kuhusu hali ya uchumi nchini, wachumi wamejitokeza kuichambua huku wakisema
Serikali iko hatarini kuua sekta binafsi.
Ripoti hiyo ya IMF ilitolewa Jumanne ikiipongeza
Serikali kwa kuimarisha uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei, kupunguza pengo
linalotokana na ununuzi wa nje ya nchi huku ikitoa hadhari kuwa Taifa
linakabiliwa na hatari itakayozuia kuendelea kukua kwa uchumi wa sekta binafsi.
Akitolea ufafanuzi ripoti hiyo juzi,
Kafulila alisema ripoti imeendelea kusisitiza eneo la ukuaji uchumi kwa kasi
nzuri ya asilimia saba, jambo ambalo alisisitiza kuwa ukuaji huo upo tangu mwaka
2005/06 ambapo uchumi ulirekodiwa kukua kwa asilimia 6.9 kwa mujibu wa hotuba
ya Bajeti ya mwisho ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa, hivyo si jambo jipya.
Alisema pia ilisisitiza kuhusu mafanikio
kwenye ukusanyaji kodi kwamba wastani wa makusanyo umeongezeka kutoka Sh
bilioni 800 kwa mwezi hadi Sh trilioni 1.1 kwa mwezi, huku mapambano dhidi ya
ufisadi yakionekana ingawa bado kuna
changamoto ya kujenga mfumo wenye nguvu ili vita iyo iwe endelevu.
Alisema ripoti hiyo ilionesha kwamba
nakisi kwenye akaunti ya biashara kimataifa imeshuka jambo ambalo ni jema na la
afya kiuchumi, lakini ripoti hiyo inakwenda mbali zaidi kuonesha kwamba nakisi
hiyo imeshuka kutokana na kupungua kwa uagizaji wa malighafi za viwanda.
“Ingekuwa nakisi imeshuka kwa kupunguza
uagizaji wa bidhaa zisizo za uzalishaji ingekuwa afya, lakini kushuka kwa
nakisi hiyo kunakotokana na kushuka kwa uagizaji wa bidhaa muhimu kwa uzalishaji
viwandani ni kasoro hasa katika mazingira ambamo Serikali inatengeneza uchumi
wa viwanda,” alisema Kafulila.
Akizungumzia
ukata, alisema ripoti ilisisitiza kuwa
uchumi unakabiliwa na ukata, na kwamba kutatua hilo, Serikali inapaswa
kuhakikisha sekta binafsi inapata mikopo ili kuchangamsha biashara, jambo
ambalo ni changamoto kubwa hasa kutokana na uamuzi wa kukopa
benki za ndani kiasi cha Sh bilioni 1,200 ili kugharimia bajeti.
Profesa Tolly Mbwete wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), alisema ripoti hiyo haiendani na namna ambavyo wananchi
wamekuwa wakilalamika kuhusu ugumu wa maisha uliopo sasa, jambo ambalo lilitokana
na Serikali kuminya mianya ya upatikanaji fedha.
Alisema sera ya Serikali kubana matumizi
ni wazi inaweza kuchangia kushuhudia kundi kubwa la wawekezaji wakifunga ofisi
zao, kwani zimekuwa zikikosa wateja, “mathalan hoteli binafsi nyingi hivi sasa
tunaona zikifungwa kwa kukosa wateja na hiyo ni kwa sababu Serikali imeagiza
watendaji wake kutumia za Serikali.
“Na ndiyo maana IMF imesema kuna hatari
kwenye sekta binafsi na utaona ni kiasi gani hali si nzuri huko, kampuni nyingi
zinafungwa, hoteli zingine zinageuzwa hosteli, matokeo yake tunapokea kundi
kubwa la watu wasio na ajira uraiani, jambo ambalo linaweza kuongeza wezi
mitaani,” alisema Profesa Mbwete.
Mhadhiri wa Uchumi wa UDSM, Haji Semboja
alisema ripoti hiyo haisemi ukweli uchumi gani umekua, kwani huu inaosemea ni
wa kawaida na umedumu kwa miaka 15 bila kubadilika kutokana na nchi yetu
kutokumbwa na ukame maeneo mengi.
“Kuna kitu kwenye uchumi kinaitwa ‘micro’
ambayo ni namna hali ya wananchi ilivyo na IMF imekuwa ikitoa ripoti hizi katika
nchi masikini na ndiyo maana inasema bei isipande kutokana na asilimia 70 ya
wananchi kuishi vijijini na ni wakulima,” alisema.
Semboja alisema ripoti ya IMF inaonesha
kuwa Serikali hailengi kunufaisha watu binafsi na ndiyo maana ikarudisha wamachinga
barabarani, jambo linaloua wenye maduka ambao wanalipa kodi, kwa sababu wateja
wengi wanadakwa na wamachinga nje ya maduka na kuwauzia bidhaa kwa bei rahisi
huku wakiwa hawana risiti hivyo kukwepa kodi.
0 comments:
Post a Comment