Frankius Cleophace, Mara
JESHI la Polisi linamsaka mkazi wa kijiji cha Kitenga
wilayani hapa, Bakari Bakari (32) kwa tuhuma za kumpiga baba yake mzazi
kichwani kwa kitu chenye ncha kali na kumsababishia kifo.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya,
Andrew Satta alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo na kumtaja aliyeuawa
kuwa ni Shaban Ramadhan (56), aliyemfumania kijana wake akiiba asali kwenye
ghala.
Satta alisema tukio hilo lilitokea Kitenga Januari 11 saa
4 usiku wakati Shaban ambaye ni mfanyabiashara wa asali, akifungua mlango wa
ghala lake kwa lengo la kuhifadhi asali.
Alisema wakati akiingia, mwanawe huyo aliyekuwa ndani ya
chumba hicho akiiba asali, alimvamia baba yake na kumpiga kichwani kwa kitu
chenye ncha kali na kumsababishia kifo papo hapo.
Mhudumu wa mochari ya Hospitali ya wilaya, Samwel Marindi
alisema siku hiyo saa 4 usiku alipigiwa simu na polisi wakimtaka afike eneo
lake la kazi kupokea mwili wa marehemu, ambao umehifadhiwa kwenye chumba hicho.
Shuhuda wa tukio hilo, Alex Chacha alisema walisikia mayowe
wakatoka nyumbani kwenda kusaidia, lakini wakakuta mwili wa marehemu kwenye
chumba alimokuwa akihifadhi asali na kupiga simu Kituo cha Polisi cha Sirari.
“Polisi walikuja wakafanya uchunguzi na kuchukua mwili
kuupeleka Bomani ulikohifadhiwa,” alisema Chacha.
Chacha ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buriba, kata
ya Sirari alisema Shaban alikuwa akikusanya asali na kuisambaza kwa wanunuzi
wilayani hapa na nje ya Tarime.
“Hatujajua kwa nini aliamua kumshambulia baba yake hadi
kumsababishia mauti, kwangu hii ni familia rafiki na ni msiba mkubwa,” alisema
Chacha.
Desemba 29 mwaka jana, Robert Mwikwabe alimpiga risasi usoni
Maite Amilly (17) mwanafunzi wa kidato cha tatu wa sekondari ya Sirari na kumuua
papo hapo wakigombea pumba za mchele.
0 comments:
Post a Comment