Leonce Zimbandu
SIKU 60 zimepita baada ya Rais John
Magufuli kukutana na Rais wa Zambia, Edgar Lungu kuzungumzia kuimarisha Mamlaka
ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA), bundi ametua upande wa Zambia baada ya
huduma ya usafiri wa treni kusitishwa kwa muda usiojulikana.
Huduma hiyo imesitishwa baada ya vyama
viwili vya wafanyakazi nchini humo kuwatangazia wanachama wao kukusanyika kutafakari,
huku wakidai marekebisho ya mishahara yao kulipwa kwa dola za Marekani.
Msemaji wa TAZARA, Conrad Simuchile alithibisha
jana kusitishwa kwa huduma hiyo alipozungumza na gazeti hili makao makuu ya
Tazara Dar es Salaam.
Alisema shughuli za usafiri wa treni ya
abiria zitaathirika upande wa Zambia kutoka Ndola hadi Kapiri Mposhi lakini
Tanzania treni za abiria na mizigo zinaendelea kutoa huduma kuanzia Dar es
Salaam hadi Mbeya.
“Mazungumzo kati ya pande mbili
yanaendelea kujadiliana na kutaka wafanyakazi warudi kazini huku majadiliano
yakiendelea, kuepusha usumbufu kwa wateja,” alisema.
Alisema mazungumzo hayo yanafanyika kati
ya Serikali, Chama cha Wafanyakazi wa TAZARA Zambia (WUTAZ) na Wafanyakazi na
Umoja wa Wafanyakazi wa Zambia (CRAWUZ) kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu.
Aliongeza kuwa kitendo cha kusitisha
usafiri kina lengo la kurudisha nyuma maendeleo ya Mamlaka hiyo, kwani tayari ilianza
kurudisha imani kwa wateja baada ya kuyumba kwa utulivu wa uendeshaji kwa miaka
mingi kupita.
Novemba 28, mwaka jana
marais Magufuli na Lungu walikubaliana kuchukua hatua madhubuti ya kuboresha
utendaji kazi wa Tazara na bomba la kusafirisha mafuta la Tanzania na Zambia
(Tazama) ili miradi hiyo ilete manufaa kwa wananchi wa Tanzania na Zambia.
0 comments:
Post a Comment