Suleiman Abeid, Kishapu
MGODI wa almasi unaomilikiwa na Kampuni
ya Williamson Diamonds Ltd uliopo Mwadui wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga,
umepongezwa kwa juhudi inazochukua katika utunzaji wa mazingira kwenye maeneo
yanayozunguka mgodi huo.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Mazingira na Uwekezaji chini
ya mwenyekiti wake Dk Dalali Kafumu.
Kamati hiyo ilitembelea mgodi huo
kukagua shughuli zinazofanyika, ikiwemo suala la utunzaji wa mazingira.
Wakizungumza na uongozi wa mgodi huo muda
mfupi baada ya kutembelea maeneo mbalimbali, wajumbe hao walieleza kuridhishwa na
utunzaji wa mazingira waliyoiona.
Wajumbe hao wameuomba uongozi wa mgodi huo
kuangalia uwezekano wa kutoa semina kwa wabunge wa ili kuwezesha kufahamu mbinu
bora za utunzaji mazingira na wazifikishe kwa wananchi wanaowawakilisha kwenye
majimbo yao.
Mwenyekiti wa kamati hiyo na mbunge wa
jimbo la Igunga mkoani Tabora, Dk Dalali Kafumu alimshauri mwekezaji huyo
kampuni ya Petra, kuandaa kupokea maombi yaliyotolewa ili kuwezesha wabunge
wote kupatiwa semina waliyoiomba.
“Kwa kweli mimi binafsi nimevutiwa na
hali ya utunzaji wa mazingira niliyoiona katika mgodi huu, mbinu zinazotumika
katika utunzaji huu sijapata kuziona katika maeneo mengine. Niwaombe wenzetu
kama itawezekana watuletee semina kule bungeni, naamini wabunge wengi wataweza
kujifunza,” alisema na kuendelea;
“Kupitia wabunge utaalamu huu utaweza
kuenea katika maeneo mengi ni mpango mzuri tumeridhishwa nao. Mbinu mnayotumia
hapa inadhibiti athari za kuzagaa ovyo kwa vumbi na pia hamkatikati miti ovyo.”
Wabunge Martha Mlacha, Faida Bakari na
Anthony Komu walielezea kuridhishwa na jinsi uongozi wa mgodi huo unavyotoa
elimu kwa jamii juu ya utumiaji wa majiko sanifu, kujitengenezea vitalu vya
miche ya miti huku mgodi wenyewe ukigawa bure kwa wananchi miti ya kupanda kwa
lengo la kutunza mazingira.
Hata hivyo, walitoa ushauri kwa mgodi
pia kuangalia uwezekano wa kusambaza zaidi kwa wakazi wa wilaya ya Kishapu
ambayo ni miongoni mwa wilaya nchini zinazokabiliwa na uharibifu wa mazingira
ili wananchi waweze kuhamasika na kupanda miti kwa wingi itakayowezesha
kurejesha uoto wa asili katika maeneo yao.
Awali, katika taarifa yake kwa wajumbe
wa kamati hiyo, msimamizi wa utunzaji wa mazingira katika mgodi huo, Donatus
Mukungu alisema katika kutekeleza kazi ya utunzaji wa mazingira, wanazingatia
na kusimamia sheria ya mwaka 2004 kuhusu uchimbaji madini unaozingatia utunzaji
wa mazingira.
“Mheshimiwa mwenyekiti kila mwaka
tunazalisha miche ipatayo 150,000 na kusambaza kwa wananchi wanaozunguka eneo
la mgodi wetu na kwa mwaka jana (2016) tuliotesha miche ipatayo 114,000
iliyotugharimu kiasi cha shilingi milioni 39, lakini pia tunatoa mafunzo ya utengenezaji
majiko sanifu ikiwemo ufugaji nyuki,” alieleza Mukungu.
0 comments:
Post a Comment