Suleiman Msuya
MKURUGENZI wa Jamii Media, Maxence Melo,
amesema kinachokuta baadhi ya Watanzania akiwamo yeye kufunguliwa kesi kinaweza
kutokea kwa waandishi wa habari siku yoyote kutokana na Sheria ya Mtandao ya Mwaka
2016 ilivyo.
Melo alisema hayo juzi wakati akichangia
semina iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Internews kuhusu Sheria ya
Takwimu ya Mwaka 2015 na Sheria ya Mtandao.
Alisema tangu awali walipinga sheria
hiyo kuwasilishwa kwa hati ya dharura na kupitishwa bila wabunge kuwa na uelewa
wa kilicho ndani yake, hali ambayo leo inaumiza watu wengi.
Mkurugenzi huyo ambaye anakabiliwa na
kesi mbalimbali, alisema ni jukumu la kila mwanahabari kutambua kinachowakuta
sasa, kuwa ni kutokana na sheria hiyo ambayo ina upungufu kadhaa.
“Kinachotokea leo ni matokeo ya vyombo
vya habari kujitoa na kuona kuwa Sheria ya Mtandao ya 2016 haitawagusa, hivyo
wakati sisi tunalalamika wanatuacha wenyewe ila nadhani kila kitu kinaonekana,”
alisema.
Melo alisema ni Tanzania pekee ambako
Jeshi la Polisi linapewa mamlaka ya kutaka kujua mtoa habari, hivyo ni dhahiri
kuwa hakuna aliye salama.
Alisema mwaka 2017 unaweza kuwa mgumu kwa
tasnia ya habari na kuwa dalili zilianza baada ya sheria hiyo kupitishwa.
Mkurugenzi huyo alisema sheria hiyo
inagusa kila eneo ambalo linahusu mawasiliano ya simu, ujumbe mfupi na hivyo
hata wanaotumia mtandao wa WhatsApp hawako salama.
Alibainisha kuwa watumiaji wa simu kwa
ujumla ni waathirika wa sheria hii bila kujali matumizi ya mtandao au simu ya
kawaida.
Akitoa mada katika semina hiyo,
Mwanasheria wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),
Deogratius Bwire alisema sheria hiyo haifai hata kipengele kimoja huku
akikitaja kipengele cha 16 kuwa chenye upungufu mwingi.
Alisema tangu sheria hiyo ipitishwe
jumla ya kesi saba zimefunguliwa na kufikisha
mahakamani zaidi ya watu 50 na wengine kuhukumiwa.
Mwanasheria huyo alisema watu walioshitakiwa
na kuhukumiwa sababu kubwa ni kuandika ujumbe kwenye kurasa zao na makundi ya
WhatsApp, hivyo waandishi wanapaswa kuwa makini.
“Watu hao walikamatwa chini ya kifungu
cha 16, kinachuzungumzia kuchapisha na kusambaza taarifa au takwimu au habari
katika mfumo wa maneno au alama,” alisema.
Alisema baadhi ya kesi ni zinazohusu
ndugu kujadili masuala ya siasa katika kundi lao la nyumbani.
Bwire aliwataja wengine walioshitakiwa kuwa
ni Erico Nyerere, Israel Willium, Habakuk Emily na wafanyakazi ambao walitumika
kama waangalizi wa TACCEO na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
“Kifungu cha 32 kinalazimisha kusaidia Polisi
kutoa taarifa za wachangiaji wa mtandao wake kama Jamii Forums, nadhani mnaona
ugumu uliopo,” alifafanua.
Aidha, alisema kifungu cha 31 kinawapa
polisi mamlaka ya kuingia bila ruhusa ya Mahakama na kuchukua kompyuta za ofisi
husika.
0 comments:
Post a Comment