Salha Mohamed
Paul Makonda |
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, ametaka madereva teksi kuwa na mita ya kuonesha umbali wa safari ya
mteja ili alipe kulingana na umbali huo na si kukadiria.
Makonda alisema hayo jana alipokutana na
madereva teksi wa Ilala ili kujadili namna bora ya kuboresha huduma hiyo.
Alisema lengo ni kutoa huduma bora za
usafiri kama Marekani na Afrika Kusini na kumfanya mteja ajue bei kuliko
kukadiria huku akiahidi kuondoa teksi bubu.
"Azma ya Serikali ni kuboresha
huduma za usafiri na kuwa wa kipekee, ili kukamilisha hilo nataka teksi
zote kutumia vifaa maalumu vitakavyoonesha umbali anaokwenda abiria,” alisema.
Aliongeza kufanya hivyo kutaondoa
gharama za ukadiriaji na kusaidia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwatoza
kodi stahiki sambamba na kuweka rangi na namba kwenye magari ili yatambulike.
Alisema ili kuboresha huduma ya usafiri
huo, ni lazima wahakikishe wanajadili mfumo bora wa uendeshaji wa biashara zao
kwa manufaa yao na abiria.
"Nawapa wiki moja mjadiliane na
mkija hapa mje na majibu ya kutatua kero zenu na namna bora ya kuendesha
biashara zenu bila bughudha," alisema.
Makonda alitaka madereva hao kuwa na
utamaduni wa kutoa taarifa wanapohisi abiria anajihusisha na matukio ya
kihalifu ili Taifa liwe salama.
"Tutaondoa teksi bubu zote, yeyote
atakayezitumia akumbuke akikumbwa na tatizo hakuna atakayemsaidia, tutaendeleza
mfumo wa kupaka rangi na kutoa namba kwa teksi zote ili kuhakikisha huduma
zinakuwa bora," alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Madereva wa Teksi
wa Ilala, Jacob Anyandwile alisema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo ni
kodi kubwa za TRA, uwepo wa huduma ya teksi kwa njia ya mtandao unafanywa na
kampuni ya UBA.
Alisema UBA imewaharibia soko kwani
kampuni hiyo inatoza bei ndogo zaidi ikilinganishwa na wao huku gharama za
uendeshaji zikiwa hazilingani, kwani hulipa kodi ndogo.
Aidha, alisema uwepo wa bajaji kinyume
na utaratibu, wamachinga kupanga bidhaa zao barabarani ni baadhi ya mambo
yanayosababisha kutofika kwa wakati maeneo wanakopeleka abiria.
0 comments:
Post a Comment