*Yajiuliza kilichojiri uchaguzi mdogo udiwani, ubunge
*Yataja
sababu tano zilizoisababishia ‘kuangukia pua’
Waandishi
Wetu
Danda Juju |
WAKATI taarifa za ndani zikionesha kuwa
kati ya kata 22 zilizofanya uchaguzi mdogo juzi, CCM imeshinda kata 21, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), vimetaja sababu
tano zilizochangia kuanguka kwenye uchaguzi huo.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana
zilieleza kuwa Chadema ndiyo iliyotetea kata hiyo, huku CUF ikipokwa moja na
kuacha maswali mengi kuhusu nguvu iliyotumiwa na vyama hivyo kwenye kampeni,
ambayo hailingani na matokeo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
JAMBO LEO jana Dar es Salaam, viongozi wa vyama hivyo walilalamikia hatua ya kuzuiwa
kwa mikutano ya hadhara na maandamano, kuwa imechangia kuanguka kwao.
Sababu nyingine ilitajwa kuwa ni kila
chama kuweka wagombea, vijana kutishwa kupiga kura na kuwaachia wazee tu,
upande wa CUF unaomwunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba kuweka wagombea na
mgogoro wa ndani ya chama hicho katika pande zote za Muungano.
Mikutano
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju,
alisema hatua ya Serikali kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya amani, ni
moja ya sababu iliyochangia Ukawa kufanya vibaya katika uchaguzi mdogo wa
marudio ya udiwani.
“Mimi binafsi haya matokeo hayajanishangaza
niliyajua, kwa sababu tangu mwanzo nilishasema, kazi kubwa ya vyama vya siasa
ni kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani yanayoonesha hisia lakini
imepigwa marufuku,” alisema Juju.
Juju alisema kwa kitendo cha kunyamazishwa
vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara na maandamano na ubabe wa Serikali
kinakwenda kuua au kunyonga vyama vya upinzani.
Alieleza kwamba wakati wao wakizuiwa,
CCM imeendelea kufanya mikutano ya hadhara kupitia wakuu wa mikoa, wilaya, Rais
na watendaji wa ngazi ya kata, ikitumia fursa hiyo kukutana na wananchi na
kuendelea kujiimarisha.
Wakati Juju analalamikia hatua hiyo ya
Serikali, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amekuwa akibeza hatua
hiyo na kusema vikao vyao vya ndani na wanachama vimewaimarisha zaidi kuliko
mikutano ya hadhara.
Kutoachiana
Akizungumzia kuhusu kutoachiana wagombea
kwenye baadhi ya kata kama utaratibu wao, Juju alisema kitendo hicho kimeonesha
udhaifu ndani ya Ukawa ambao wanatakiwa kuuchukua kama changamoto na kuifanyia
kazi ili kujiimarisha.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kushindwa kwao kwenye uchaguzi huu kumesababishwa
kwa kiasi kikubwa na mienendo ya Serikali kutisha vijana, hivyo kushindwa
kujitokeza kupiga kura.
Shaweji alitaja sababu nyingine kuwa vijana
kutojitokeza kwenye uchaguzi, kwa sababu ya kukata tamaa na kutokana na hali
hiyo, wamekuwa wakirubuniwa na kutoa vitambulisho vyao kwa kupewa ‘bahasha’ na
CCM ili wasijitokeze.
Alisema kutokana na hali hiyo, wanaojitokeza
kupiga kura ni wachache ambao ni wanawake na wazee kwa kuwa wakati mwingine
vijana wanaona hata wakijitokeza, vyama vya upinzani haviwezi kushinda.
Akizungumzia suala la kutoachiana baadhi
ya kata, alidai Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba na timu yake, ndio
walivuruga utaratibu kwani wao walisema hawatashirikiana na Ukawa na hivyo
kuweka wagombea katika kata zote.
Kutokana na hali hiyo, Shaweji alisema walijikuta
vyama vingine vya Ukawa vikiweka wagombea kwenye kata hizo wakiwa na lengo la
kuivuruga CUF ya Lipumba isishinde.
“Kwa mfano kata ya Kijichi, CUF
ilionekana kuwa na nguvu tangu uchaguzi uliopita, lakini vyama vingine viliweka
wagombea ili kuivurugia CUF isishinde,” alisema Mketo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema matarajio yao yalikuwa ni
kushinda kwa kishindo, lakini matokeo yamekuwa kinyume.
“Unapoingia
kwenye uchaguzi, unaamini unakwenda kushinda na si kushindwa, kwa hiyo
matarajio yetu yalikuwa nji kushinda tena vizuri sana,” alisema Mwalimu.
Aliongeza
kuwa hawezi kusema sababu zilizochangia kushindwa kwao kwa kuwa bado hawajapata
mrejesho wa hali ilivyokuwa kutoka kata mbalimbali, ili kufanya tathmini.
Mgogoro CUF
Wakati
huo huo, Jumuiya
ya Vijana ya CUF (Juvicuf), imesema mgogoro unaondelea ndani ya chama hicho umesababisha kufanya vibaya kwenye
uchaguzi huo.
Kutokana
na hali hiyo, Juvicuf imewataka vijana wote wa chama hicho kurudi nyuma na
kutafakari hatima ya chama chao na wasipofanya hivyo, upo uwezekano wa uchaguzi
wa mwaka 2020 ‘kuwawashia taa nyekundu’.
Mwenyekiti
wa Juvicuf ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobal alisema hayo jana
alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Bobal
alisema hakuna sababu ya wanachama wa CUF kutafuta mchawi kutokana na matokeo
hayo, kwani ushahidi upo wa kutosha kuwa mgogoro uliopo unakimaliza chama.
Alisema
mgogoro wa CUF ulikuwa ni kati ya Profesa Lipumba na chama, ila kwa sasa umeongeza
maadui ambao ni vyombo vya Dola na CCM, jambo linalozidi kuharibu chama.
Mwenyekiti
huyo alisema pamoja na mikakati ambayo inaongozwa na makundi hayo, bado wana
CUF hasa vijana wana wajibu wa kutafakari na kuchukua uamuzi kuhusu chama chao
na wao pia.
“Mimi
na wenzangu katika jumuiya tumekaa na kutafakari kwa dhati na kubaini kuwa
mgogoro ndani ya chama chetu hivi sasa umepata
mashabiki wengi ambao hawakitakii mema, chama kinapambana na Dola, CCM na sisi
kwa sisi,” alisema.
Alisema
kwa wingi huo wa maadui chama kupata matokeo hayo si jambo la kushangaza, hali
inayowaumiza vijana, hivyo ni vema kutafuta njia ya kukinusuru.
“Tunatoa
mwito na kufungua milango kwa vijana wa CUF, kutafuta njia ya kukinusuru chama
badala ya kukubali kutumika kukiangamiza kwa lengo la kumfurahisha mtu mmoja,”
alisema.
*Imeandikwa na Suleiman Msuya na Abrahama Ntambara.
0 comments:
Post a Comment