Abraham Ntambara
WAKATI CUF
leo ikiadhimisha miaka 16 ya kumbukizi ya mauaji na ukiukwaji wa haki za
binadamu, imeihadharisha CCM na Rais John Magufuli kutofanyia mzaha matumizi
makubwa ya nguvu za Dola kuendesha shughuli za kidemokrasia na uchaguzi nchini.
Taarifa
iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu
na Sheria wa CUF, Pavu Abdallah Juma, ilisema
wanalaani mauaji ya raia wasio na hatia na vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki
za binadamu vilivyofanywa na Serikali ya CCM.
“Jeshi
la Polisi limeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa misingi ya haki, sheria na
uadilifu, badala yake linatumika kama mkono wa kulazimisha ushindi
wa CCM katika uchaguzi na kufanya kazi zake kisiasa zaidi, badala ya kutanguliza
uzalendo na weledi,” alisema Juma kwenye taarifa hiyo.
Aidha,
iliitaka Serikali kutambua kuwa wananchi wamechoka uonevu na ukiukwaji wa haki
za binadamu na wamechoka kunyanyaswa na kushindwa kuheshimiwa kwa mfumo wa
siasa za vyama vingi nchini, misingi ya demokrasia na uchaguzi huru na wa haki.
Iliionya
Serikali ya CCM na vyombo vya Dola kutoirejesha nchi kwenye matukio ya Januari
26 na 27, 2001 ambayo yalisababisha umwagaji wa damu na mauaji ya raia wasio na
hatia.
Alisema CUF
itaendeleza juhudi za kuhakikisha migogoro ya kisiasa inapata ufumbuzi kwa njia
ya kidemokrasia na amani, na kuunganisha Wazanzibari na Watanzania kwa kuwa kitu kimoja na kutanguliza maslahi mapana
ya nchi.
Aidha, ilitoa
shukrani kwa viongozi, wanachama, wapenzi na wananchi wakazi wa Zanzibar
kwa uvumilivu ambao unadhihirisha
ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa, licha ya hujuma, mauaji, uchokozi na
usumbufu wa makusudi uliofanywa na Jeshi la Polisi na vyombo vya Dola na vikosi
vya ulinzi.
Taarifa
ilieleza kuwa CUF itaendelea kushirikiana na vyama vingine vya siasa, wadau
wanaounga mkono kuheshimiwa kwa demokrasia na misingi ya utawala bora ili
kuhakikisha Serikali ya CCM inaheshimu demokrasia na Watanzania wanapata tume huru za
uchaguzi na Katiba inayotokana na ridhaa yao.
Ilibainisha,
kwamba madai hayo yanaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa ambayo ilishiriki kwenye
uangalizi wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka juzi, ambapo katika ripoti ya waangalizi wa Jumuiya
ya Ulaya walipendekeza hadi 2020 matatizo yaliyopon yawe yamefanyiwa kazi.
Mwaka
2001 wanachama na wafuasi CUF walijitokeza kwenye maandamano ya kupinga matokeo
ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 na kudai Katiba mpya na tume huru za uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment