*Ni baada ya kuteliwa kuwa balozi
*Asisitiza
hakuna Katiba kukiukwa
Salha
Mohamed
Dk Abdallah Possi |
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Wenye Ulemavu, Dk
Abdallah Possi, amesema wakati wowote atakabidhi barua ya kujiuzulu ubunge kwa
Spika Job Ndugai.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Rais
John Magufuli kumteua kuwa balozi.
Dk Possi ambaye pia ni mwanasheria aliweka
wazi jana kuwa hakuna sheria itakayovunjwa kutokana na uteuzi wake kuwa balozi
na kuwatoa hofu Watanzania.
Kauli ya Dk Possi kuwa ataandika barua
ya kujiuzulu ubunge imekuja wakati kuna mjadala mkubwa ukidai kuwa uteuzi wake
umetokana na hoja za kisheria kwamba Katiba ilikiukwa baada ya Rais kuteua
wabunge wawili; Abdallah Bulembo na Profesa Palamagamba Kabudi.
Baada ya uteuzi wa wabunge hao juzi,
Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu
aliueleza umma kuwa watakwenda kupinga bungeni wateule hao, kwani kikatiba Rais
kwenye nafasi zake 10 za uteuzi anatakiwa ateue wabunge wanawake angalau watano,
lakini waliopo sasa ni wawili na kubaki na nafasi mbili tu.
Hata kama angejaza nafasi hizo kwa
kuteuia wanawake bado asingefikisha idadi ambayo inatakiwa na Katiba kwani
wangekuwa wanne.
Wakati mjadala huo ukiendelea, juzi
usiku, taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari ilisema Rais alimteua Dk Possi
kuwa balozi, hatua iliyoonekana ni ya kutaka kutengeneza nafasi tatu kwa ajili
ya kukamilisha idadi hiyo ya wanawake iwapo italazimika.
Akizungumza jana baada ya kuteuliwa na Rais,
Dk Possi alisema hatua iliyopo mbele yake ni kuandika barua ya kujiuzulu na si
vinginevyo kwa kuwa anaheshimu imani ya Rais kwake.
“Inawezekana
kuandika barua ya kujiuzulu hakuna anayenikataza kufanya hivyo,” alisema baada
ya mwandishi wa habari hii, kutaka kufahamu kama ameshaiandika na kuiwasilisha
kwa Spika Ndugai.
“Bado… inaweza ikawa niiandike sasa hivi
(jana), kubwa ni kwamba siwezi kuendelea kuwa mbunge, kwa hiyo naweza kuandika
barua leo (jana), kesho(leo) au Jumatatu,” alisema.
Alisema kwa uteuzi huo hawezi kuendelea
kutumikia nafasi mbili kwa wakati mmoja.
Possi alisema kama alivyoteuliwa
kutumikia wananchi, atawakumbuka kwani amewatumikia kwa mwaka mmoja na kujifunza
mengi.
“Unapokuwa kwenye jamii, unakutana na
watu na unapoondoka utawakumbuka lakini mwisho wa siku nilikuwa mtumishi
nahudumia Taifa, hivyo hii ni nafasi nyingine ya kuhudumia nchi,” alisema.
Alisema katika mwaka mmoja amejifunza
vingi na mawaziri, wabunge hivyo ataendelea kutumia aliyojifunza.
Alisema katika nafasi aliyoteuliwa,
hajui atakutana na changamoto zipi mpya kwani atakutana na watu wengi katika
kujifunza.
“Tusubiri kila kitu kitakuja kwa wakati
wake na hakuna sheria itakayovunjwa, we subiri katika hiki kitakachoendelea,
lakini hakuna Katiba wala sheria itakayovunjwa,” alisema.
Alisema Watanzania wasubiri siku chache
zijazo kila kitu kitakuwa sawa.
Spika Ndugai alipotafutwa kufahamu kama
amepokea barua ya kujiuzulu kwa Dk Possi, alisema kwa sasa yuko jimboni na kama
kuna barua ataikuta bungeni.
“Mimi hata bungeni sipo, niko jimboni,
kama kuna barua nitaikuta huko huko nitakapokwenda bungeni Januari 31,” alisema.
Kuteuliwa kwa Profesa Kabudi na Bulembo,
kuliamsha hisia kwa baadhi ya watu kwamba kwa vyovyote Rais atafanya mabadiliko
kwenye Baraza lake la Mawaziri, hatua ambayo hivi sasa haiepukiki kwani nafasi
ya Possi itatakiwa kujazwa.
Uteuzi wa wawili hao ulifanya sasa Rais
abaki na nafasi mbili za uteuzi lakini kutokana na Possi kuteuliwa kuwa balozi,
inaongezeka moja ambapo kwa vyovyote kikatiba zitatakiwa kujazwa na wanawake,
ili kutimiza matakwa ya ‘angalau’ watano.
0 comments:
Post a Comment