Waandishi Wetu
Baraza la Mawaziri |
RAIS John Magufuli anatarajia kuipanga
safu yake ya Baraza la Mawaziri wakati wowote, huku baadhi ya naibu mawaziri na
wabunge aliowateua wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mawaziri.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa
kumteua aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Dk Abdallah Posi kuwa balozi na hivyo
kufanya nafasi hiyo kubaki wazi.
Historia inaonyesha kuwa Rais
Magufuli amekuwa na utaratibu wa kuwapa
uwaziri wabunge ambao amewateua.
Ukiacha Posi ambaye aliteuliwa kuwa
mbunge na kisha waziri, wabunge wengine walioteuliwa na kiongozi mkuu huyo wa
nchi na kuteuliwa kuwa mawaziri ni;
Profesa Joyce Ndalichako (Elimu), Dk Agustino Mahiga (Mambo ya Nje),
Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano) na Dk Philip Mpango
(Fedha) huku Dk Tulia Ackson ambaye naye
aliteuliwa kuwa mbunge, akichaguliwa kuwa Naibu Spika.
Wiki iliyopita Rais Magufuli aliteua
wabunge wawili, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo na
nguli wa sheria, Profesa Paramagamba
Kabudi.
Kutokana na utaratibu huo na uzoefu wa
wateule hao, wachambuzi waliozungumza na gazeti hili walisema huenda Profesa
Kabudi na Kilango wakateuliwa kuwa mawaziri.
Katika orodha hiyo, Kilango ambaye
alikuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga
ametajwa kutokana na kuwa miongoni mwa wateule saba wa Rais, ambao kati
yao sita wamepewa wizara.
Wachambuzi hao wamesema pia nafasi ya
Posi inaweza kuzibwa na mbunge mlemavu
kwa maelezo kuwa historia inaonesha kuwa akiondolewa waziri kutoka ukanda
fulani, atateuliwa wa kutoka ukanda huo huo, iwapo aliyeondolewa alikuwa
mlemavu, basi atarejeshwa mlemavu.
Kauli za wasomi
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Profesa Mwesiga Baregu alisema,
“Rais Magufuli si mtu anayetabirika kwa sababu hakuna aliyeamini kuwa
atamrejesha Kilango bungeni na kumteua Posi kuwa balozi. Kuna uwezekano mkubwa
nafasi ya Posi ikajazwa na Profesa Kabudi maana ni mwanasheria pia.”
“Ingawa Kabudi ana nafasi lakini huwezi
kuwapuuza wabunge wengine. Huenda Magufuli akateua miongoni mwao kuziba nafasi
ya Posi.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Benson Bana alisema litakuwa jambo
jema iwapo Rais Magufuli atamteua mlemavu kuziba nafasi ya Posi, huku akimtaja
mbunge wa viti maalum (CCM), Amina Mollel.
“Ikiwa atafanya hivyo itakuwa vizuri zaidi.
Binafsi naona mabadiliko makubwa katika baraza la mawaziri. Naona wazi uwepo wa
Profesa Kabudi katika baraza la mawaziri maana ni hazina ya taifa amejaliwa
kipaji cha kufikiri cha hali ya juu,” alisema.
Vigezo uwaziri
Ikiwa Rais Magufuli ataendeleza
utaratibu wa mtangulizi wake wa kuteua waziri kutoka mkoa anaotoka waziri
aliyeondoka, wabunge kutoka mikoa ambayo mawaziri wataoondolewa, wataula katika
uteuzi huo.
Nani kubaki?
Wakati ikisubiriwa mabadiliko hayo wapo
baadhi walikuwa mawaziri katika Serikali iliyopita, kufanikiwa kuteuliwa tena
katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Mawaziri hao ni Profesa Jumanne
Maghembe, Profesa Sospeter Muhongo, William Lukuvi, Dk Hussein Mwinyi, Profesa
Mbarawa, Dk Tizeba, Gerson Lwenge, Charles Mwijage, Jenister Mhagama, Mwigulu
Nchemba, Ummy Mwalimu, Angela Kairuki, January Makamba, George Simbachawene na
Dk Harrison Mwakyembe.
Miongoni mwao, Dk Mwinyi amefanikiwa
kuwemo ndani ya baraza la mawaziri bila
kutoka nje ya uwanja.
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa waziri
aliyeshughulikia masuala ya Muungano, mwaka 2008 alipewa kuongoza Wizara ya
Ulinzi na mwaka 2012 aliteuliwa kuiongoza Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Mwingine ni Profesa Jumanne Maghembe,
mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, nafasi aliyoishika kwa miaka miwili
hadi mwaka 2008 alipokabidhiwa mikoba ya kuiongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi. Mwaka 2010 alipewa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kabla ya
kuhamishiwa Wizara ya Maji anayoiongoza hadi hivi sasa.
0 comments:
Post a Comment