Aidan Mhando, Geita
WACHIMBAJI wadogo 14 wa mgodi wa dhahabu wa RZ wa kata ya
Nyarugusu mkoani hapa, akiwamo raia wa China, wamefunikwa na kifusi cha udongo kutokana
na maporomoko kwenye moja ya mashimo walilokuwa wakichimba.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya
wachimbaji wenzao zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 9 alfajiri
wakati wachimbaji hao wakiendelea na uchimbaji wa dhahabu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel
Kyunga ambaye alikuwa ziara ya kikazi mkoani humo, alisitisha ziara yake ili
kutembelea eneo la tukio.
Kyunga aliagiza uokoaji uanze mara moja na kubainisha
kuwa hadi anaondoka eneo la tukio, ulikuwa ukiendelea bila mafanikio kutokana
na kutofikiwa kwa wachimbaji hao.
Tukio hilo lilitokea takribani miezi 14 tangu wachimbaji watano
wa mgodi wa Nyangarata, Kahama mkoani Shinyanga, kuokolewa wakiwa hai baada ya kufunikwa
na kifusi cha udongo ardhini kwa siku 41.
Wachimbaji hao waliokolewa Novemba 16 mwaka juzi, baada
ya kufunikwa Oktoba 5 na kubainisha kuwa waliishi siku hizo zote kwa kula
wadudu kama mende na mizizi huku wakitumia kofia kukinga maji yaliyokuwa
yakitiririka kutoka juu na kunywa.
Watu walioshuhudia tukio hilo lililoacha kumbukumbu ya aina
yake nchini, walisema ardhi ya juu ya machimbo hayo ilititia na kuporomoka kutokana
na mvua iliyonyesha na kuwafunika. Katika jitihada za uokoaji, waliokolewa
wachimbaji watano.
0 comments:
Post a Comment