Fidelis Butahe
SIKU moja baada ya CUF kuanika jinsi Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa ilivyobariki kambi inayoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba
kuchukua Sh milioni 369.4 za ruzuku, chama hicho kimesema kinasubiri Rais John
Magufuli atengue uteuzi wa Jaji Francis Mutungi.
Kimesema kutokana na Rais Magufuli kuwa mstari wa mbele
kupambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu, kinaamini hatasita kumchukulia
hatua Jaji Mutungi kwa madai kuwa amebariki ubadhirifu na utakatishaji wa fedha
kinyume na sheria.
“Tunasubiri kuona kama atamtumbua au la au atampandisha cheo.
Awali (Mutungi) alizuia ruzuku kutoka, iweje sasa aitoe wakati chama kina
mgogoro? Tunajadiliana ikishindikana tutampeleka mahakamani, licha ya kuwa
tayari tumemfungulia kesi na inaendelea,” alisema Nassor Ahmed Mazrui, Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar.
Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho,
Julius Mtatiro alisema ruzuku hiyo iliyokuwa imezuiwa na Ofisi ya Msajili
imeanza kutoka na mnufaika ni Profesa Lipumba ambaye anatambuliwa na ofisi
hiyo.
Alisema kitendo hicho kimefanywa na viongozi wanaomuunga mkono
Profesa Lipumba, watendaji wa Serikali na maofisa wa benki iliyotoa fedha hizo.
Mtatiro alisema wanachama wanaomuunga mkono Profesa
Lipumba walichukua fedha hizo kupitia akaunti ya CUF Temeke, kisha
wakazihamishia kwenye akaunti binafsi tofauti, wakati fedha za ruzuku huwekwa
kwenye akaunti kuu inayosimamiwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
“Ni kudhihirisha namna gani Msajili anavyotumika. Yeye
ndiye alileta mgogoro CUF kwa kuridhia Lipumba aendelee kuwa mwenyekiti. Oktoba
10 alisitisha ruzuku kutokana na mgogoro wa kiuongozi uliokikumba chama, ila
bila chochote ameruhusu fedha kutoka,” alisema Mazrui.
“Fedha zimetoka kinyume na taratibu na sheria. sijui kwa
kweli labda naye ana mgao wake.”
Alisema kutokana na hali hiyo, wanasubiri hatua za Rais
Magufuli dhidi ya Msajili huyo na kusisitiza kuwa iwapo kiongozi mkuu wa nchi atasita
kumtumbua Jaji Mutungi, atakuwa anadanganya Watanzania.
“Rais Magufuli anapigania haki na kutetea wanyonge na
masikini. Katika hili ajitokeze na kumchukulia hatua Msajili. Kama anapigania haki
ya wanyonge achukue hatua katika hili,” alisema.
Jana gazeti hili lilimtafuta Jaji Mutungi ambaye awali
aliahidi kufuatwa ofisini kwake, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo na mengine
lakini badala ya kutoa ufafanuzi, alisema ana shughuli nyingi atafutwe siku
nyingine.
Kuhusu kesi, Mazuri alisema licha ya kuwa kesi ya awali
ipo mahakamani, chama hicho kitajadili kwa kina uamuzi huo na wajumbe
wakikubaliana, watamfungulia kesi nyingine Msajili.
“Tutaitisha vikao vya Kamati Tendaji na Baraza Kuu la
Uongozi, vikiamua tutamshtaki. Vikao hivyo vitafanyika siku za karibuni, si
unajua hatuna ruzuku hivyo lazima tuchangishane, tutafute mahali mwafaka pa
kufanyia,” alisisitiza.
Oktoba mwaka jana, Bodi ya Wadhamini CUF ilifungua kesi Mahakama
Kuu. Katika kesi hiyo, Bodi inaiomba Mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya
Msajili inayomtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Pia, wanaiomba Mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili
kufanya kazi nje ya mipaka yake ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake
na pia itoe amri ya kumzuia kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya chama
hicho.
0 comments:
Post a Comment