Aidan Mhando, Mwanza
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela amewasimamisha
kazi watendaji watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani hapa, ili
kupisha uchunguzi wa matumizi ya fedha zaidi ya sh. milioni 300, zilizotolewa
na Benki ya Dunia kwa ajili ya maendeleo wilayani humo.
Waliosimamishwa kazi ni pamoja na mweka
hazina, mchumi na Mhandisi wa Halmashauri hiyo. Kwa pamoja wanadaiwa kubadili
matumizi ya fedha za kutekeleza miradi ya SEDEP, zilizotolewa na benki hiyo kwa
ajili ya kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi wa shule za sekondari.
Akizungumza akiwa katika ziara wilayani
humo juzi, Mongela alisema ni lazima uchunguzi wa kina ufanyike, kwani thamani
ya vyumba vya madarasa na vyoo vilivyojengwa kutokana na fedha za mradi huo,
hailingani na fedha zilizotumika.
“Kunzia Jumatatu (leo), kuna timu ya
wakaguzi itakuja hapa Magu kukagua na kuchunguza thamani ya fedha zilizotumika
kwenye miradi hii ambayo nimeikagua. Miradi hii inajumuisha miradi ya ujenzi wa
vyumba vya madarasa na vyoo ambayo inaonyesha wazi kuna uchakachuaji
umefanyika,”alisema Mongela.
Mkuu Wilaya ya Magu, Hadija Nyembo
alisema mambo yaliyokwamisha miradi ya ujenzi huo ni kuelekeza fedha hizo
katika ujenzi wa maabara tofauti na matumizi ya fedha yalivyopangwa.
Hata hivyo, mabadiliko ya matumizi ya
fedha hizo, yanadaiwa kuwa yalifanyika bila kuthibitishwa na Wizara ya Fedha
na Mipango ili yapewe baraka kwa kuwa Wizara hiyo, ndio yenye mamlaka ya kutoa
idhini ya mwisho ya matumizi ya fedha za Umma.
Kutokana na sababu hizo mkuu huyo wa
Mkoa aligoma kuzindua vyumba viwili vya madarasa vya shule ya msingi Nyanguge
vilivyojengwa kupitia kiasi hicho cha fedha, kutokana na madai kuwa vyumba
hivyo pamoja na ujenzi wa vyoo vimejengwa chini ya kiwango.
0 comments:
Post a Comment