Mashaka Mgeta
JUNI 23 mwaka jana, Rais John Magufuli alipokea ripoti ya
Uchaguzi Mkuu wa 2015 kutoka kwa Mwenyekiti (mstaafu) wa Tume ya Taifa ya
uchaguzi (Nec), Jaji mstaafu Damian Lubuva.
Hafla ya kuipokea ripoti hiyo ilifanyika Ikulu jijini Dar
es Salaam, Rais Magufuli akazungumzia masuala tofauti ikiwapo kusitisha
shughuli za kisiasa hususani mikutano ya hadhara na maandamano.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli akasema ni wakati wa
‘hapa kazi tu’, hivyo wananchi waachwe wafanye kazi pasipo kuingiliwa na
masuala ya siasa, wakati Serikali yake ikitekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa
kampeni za Uchaguzi Mkuu huo.
Hoja nyingi zilitolewa kumsifu na kumpongeza Rais
Magufuli kwa hatua hiyo, kama ilivyokuwa kwa wakosoaji wake walioelezea
kukandamizwa kwa misingi ya demokrasia.
Lakini tangu Rais Magufuli apige marufuku mikutano ya
hadhara, kisha kutolewa kwa tamko la jeshi la polisi hakuna chama ama
mwanasiasa aliyekiuka maagizo hayo, isipokuwa kwa kufanya vikao vya ndani kwa
chama husika.
Kutoka Juni 23, mwaka jana Rais Magufuli alipotoa tamko
la kuzuia shughuli hizo za siasa, hadi Desemba 23 mwaka jana ilipoanza mikutano
ya kampeni za udiwani ikawa takribani siku 30 zilizotoa mwanya kwa wanasiasa wa
upinzani angalau kuwa huru kwenda sehemu tofauti za nchi wakishiriki na
kuhutubia mikutano ya hadhara.
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akasema
ulikuwa ni wakati muafaka kwa wapinzani kuzitumia kampeni hizo kwa ajili ya
kuzungumza na wananchi masuala ya kitaifa, kwa vile zilipofikia ukomo wake
Januari 21, mwaka huu, wangerudi kwenye ukimya kwa maana hapatakuwa na mikutano
ya hadhara.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini kupitia chama
hicho, anathibitisha kuwa agizo la Rais Magufuli na hatua ya polisi kusitisha
mikutano ya hadhara ya kisiasa litaendelea kufuatwa baada ya uchaguzi wa
udiwani wa marudio wa ubunge katika jimbo la Dimani kufanyika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akakaririwa akisema ukimya wa wapinzani
unaotokana na maagizo hayo hauwaathiri wanasiasa pekee bali jamii nzima kwa
vile inanyimwa uhuru wa kujieleza.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu anasema kampeni za udiwani na ubunge zilitoa
mwanya wa uhuru katika kufanyika kwa mikutano ya hadhara isiyoweza kuzuiwa.
Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, akasema ni
kutokana na hali hiyo wanasiasa hasa wa upinzani walizitumia kampeni za
uchaguzi huo kuzungumzia masuala tofauti hususani matatizo yanayolikabili Taifa.
MIKUTANO YA NDANI
Mara kadhaa, viongozi wa upinzani akiwamo aliyewahi kuwa
Waziri Mkuu ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Ed-ward
Lowassa, wamekuwa wakiisifu kuwa ni yenye kuwaimarisha na kuwajenga zaidi.
Hoja hiyo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, akisema mikutano ya ndani
bado inawanufaisha kwa vile inatumuka kuikosoa Serikali na ujumbe kuwafikia
wananchi.
Hata hivyo, Mtatiro anaamini kuwa pamoja na katazo la
Rais Magufuli na polisi kuhusu mikutano ya hadhara, mabadiliko ya sayansi na
teknolojia ya mawasiliano yanawawezesha (wapinzani) kufikisha ujumbe kwa jamII
Pana kama inavyofanyika katika nchi nyingine duniani.
“Tunaweza hata kutumia mitandao ya kijamii na hizi kampeni
za uchaguzi mdogo kufikisha ujumbe kwa umma. Sioni kama kuna njia mtu anaweza
kuitumia kwa sasa kuvizuia vyama vya upinzani kuzungumzia matatizo ya
wananchi,” akasema.
Lakini wapo wanasiasa wanaoamini kwamba kuwapa wapinzani
fursa ya kuzungumza na kusikika kwenye jamii, kunasaidia kuyajadili na kupata mawazo
mapya ya kukabiliana na kero zilizopo nchini.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, anasema
wapinzani wanapozuiwa kutoyazungumzia matatizo ya nchi ni sawa na kuashiria
kutohitaji kadhia hizo kujulikana na kusikika.
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, akasema hakuna
haja ya kuwazuia wapinzani kufanya shughuli za siasa hususani mikutano ya
kampeni kwa vile baadhi ya mambo yanayotekelezwa na Serikali, yamo kwenye ilani
ya uchaguzi.
Sumaye anasema masuala yaliyopo kwenye ilani ya Chadema
ya mwaka jana, hayana athari kwa Taifa na ndio maana miongoni mwa hayo
yanatekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.
MIKUTANO ILIVYOZUIWA
Rais Magufuli alitoa kauli ya kupiga marufuku mikutano ya
wanasiasa alipokuwa akizungumza Ikulu Dar es Salaam, baada ya kukabidhiwa
ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani
kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kama
tumeyatekeleza au hatujayetekeleza,” akasema.
Rais Magufuli alisema hatua hiyo ni sahihi kwa vile hata
nchi zilizobobea kwenye misingi ya demokrasia (hakuzitaja), haziendelezi siasa baada
ya uchaguzi na badala yake kuwekeza katika kufanya kazi.
Akasema, “haiwezekani mkawa kila siku ni siasa watu watalima
saa ngapi, kila siku ni siasa, ni vema tukatimiza wajibu wetu tuliopewa na
wananchi na watatupima kwenye hilo.”
Rais Magufuli akaelezea matumaini yake kuwa Watanzania
wanachokihitaji kwa wakati huu ni maendeleo.
Rais Magufuli akasema katika kampeni za 2015, aliahidi
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kipindi cha miaka mitano, hivyo
asingependa kuona mtu yeyote anamchelewesha katika utekelezaji.
USHAURI
Rais Magufuli akashauri kuwa kama kunan hitaji la kuwapo
mikutano ya hadhara, isiwe kwa wanasiasa wakiwamo wabunge kutoka majimbo
mengine kwenda kuungana na mbunge wa jimbo husika kuwahutubia wananchi.
Badala yake akasema kila mbunge na diwani anapaswa
kufanya mkutano ndani ya eneo lake la uwakilishi. Akatoa mfano akisema, “kama
ni madiwani wakapeleke hoja kwa nguvu zote kwenye maeneo yao, kama ni wabunge
wakazungumze kwa nguvu sana bungeni lakini hata kuziba midomo nayo ni demokrasia,
hiyo ni demokrasia ya mwelekeo wa ya aina yake.”
KUSHIRIKIANA NA WAPINZANI
Rais Magufuli akasema Serikali yake imeamua kufanya kazi
kwa kushirikiana na vyama vyote vya
siasa ili kuchagiza kasi ya kutatua kero za wananchi.
Katika kuthibitisha hilo, akasema atashirikiana na
wanasiasa katika changamoto ambazo utatuzi wake utasaidia kulijenga taifa.
0 comments:
Post a Comment