Celina Mathew
Julius Mtatiro |
MGOGORO wa CUF umechukua sura mpya, baada ya kila upande
kuanza kutoa siri za ndani za matumizi mabaya ya mamilioni ya rukuzu za chama
hicho.
Aliyeanza kuweka wazi siri hizo hadharani ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro, anayeunga mkono upande Katibu Mkuu,
Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alieleza namna ruzuku ya Sh milioni 369,
ilivyochukuliwa kinyume na taratibu.
Juzi Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya
Umma CUF, Abdul Kambaya, anayeunga mkono upande wa Mwenyekiti, Profesa Ibrahim
Lipumba, aliamua kuweka hadharani uchotaji mwingine wa mamilioni ya chama hicho
unaodaiwa kufanywa na Mtatiro na kujibiwa.
‘Uchotaji’ wa Mtatiro
Kambaya katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alidai
kuwa Mtatiro alipokuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, aliwahi kuingizia zaidi ya Sh
milioni 108 za chama hicho kwenye akaunti yake iliyopo NMB, yenye namna 5091603335.
Kwa mujibu wa madai ya Kambaya, Septemba 5 mwaka 2011 Mtatiro
alianza kutoa fedha hizo kidogokidogo, kwa kuhamisha Sh milioni 34.09; Septemba
13, 2011 alihamisha Sh 270,000 na Septemba 19, 2011 alihamisha Sh. milioni 24.87.
Kambaya aliendelea kudai kuwa Septemba 27, 2011 Mtatiro, alihamisha
Sh milioni 30.87 na Septemba 30, 2011 kiongozi huyo alihamishsa Sh milioni 10,85
huku Oktoba 3 akihamisha Sh. milioni nane na kumaliza kuhamisha Sh 108,959,500.
"Huyu ndie Julius Mtatiro ambae anataka kujifanya
mtakatifu kumbe ndie mtakatishaji namba moja wa fedha za CUF. Je wakati Julius
anahamisha fedha hizi kutoka akaunti ya CUF na kuingiza kwenye akaunti yake
binafsi, alikua hujui kwamba fedha za taasisi haziruhusiwi kuhamishiwa kwenye
akaunti binafsi? Alihoji.
Akitoa ufafanuzi kuhusu akaunti namba 414016000207 ya Mhina
Omary Masoud iliyopo NMB, Kambaya alidai mwaka 2012 Mtatiro alipokuwa Naibu
Katibu Mkuu Bara, alimwingizia mtu huyo huyo Sh milioni 47.
Kambaya alisema uwekaji wa fedha za ruzuku za CUF katika
akaunti ya Mhina Omary Masoud, haukuwa jambo geni kiasi cha kumfanya Mtatiro
ashangae na kujifanya hamjui mwenye akaunti hiyo.
Kiongozi huyo anayeunga mkono ypande wa Lipumba, alidai
kuwa Mtatiro anajua kuwa akaunti hiyo pia ili wahi kupatiwa fedha chini ya
uongozi wake lakini hukuwahi kuitisha mkutano wa vyombo vya habari na kuelezea
umma juu ya ukiukwaji huo wa taratibu za fedha za taasisi.
Alidai katika taarifa yao kwa vyombo vya habari kuhusu
kadhia hiyo, walisisitiza kuwa Mtatiro si kiongozi wa CUF, hivyo si sahihi yeye
kutoa taarifa kuwa CUF imeibiwa mamilioni na pia haikua sahihi kusema fedha
hizo zimeibwa kutoka Hazina.
"Julius Mtatiro na genge lake ni wapiga dili
waliokosa nafasi ya kutimiza matakwa yao ndani ya CUF na si miongoni mwa
viongozi wanao weza kuwa waadilifu,"aliongeza Kambaya.
‘Uchotaji’ wa Kambaya
Akijibu tuhuma dhidi yake zilizotolewa na Kambaya,
Mtatiro naye aliamua kuanika namna Naibu Mkurugenzi huyo wa Habari, vyokimbia
na fedha za kampeni za Igunga.
Katika taarifa yake ya jana, Mtatiro alidai kuwa Septemba
20 mwaka 2011, wakati wa kampeni za Igunga, Kambaya alisaini Sh milioni 2.2 za kujikimu
kwa ajili ya kusimamia mambo maalum waliyokubaliana kwenye zoni yake ya
kampeni.
Mtatiro alidai kuwa Kambaya baada ya kusaini fedha hizo,
alitokomea Dar es Salaam na kuitelekeza Zoni muhimu ya kampeni za Igunga bila kukiaga
chama wala Katibu Mkuu, na hakurudi Igunga tena.
“Nilipokwenda kwenye Zoni husika baada ya siku tano,
ndipo nakaambiwa Kambaya ametokomea. Ikabidi nimpigie simu hakupokea na
nikachukua hatua za kumpandisha ndugu Mohammed Marjeby (aliyekuwa Mwenyeji wa
Zoni) ili achukue nafasi ya Kambaya,”alidai.
Alidai baada ya Kambaya kutoroka na fedha hizo hadi leo,
hakuwahi kuzirejesha na kwamba alichofanya ni kumjulisha Katibu Mkuu na
Mwenyekiti.
Pia alidai kuwa hata mwaka juzi (wakati wa Uchaguzi Mkuu),
Kambaya alipangiwa usimamizi wa kampeni katika maeneo kadhaa ya nchi,
akakabidhiwa Sh. milioni 3 na hakwenda kwenye kampeni hizo.
Utetezi wa Mtatiro
“Wizi ni tabia tu na hata Kambaya akijaribu kuangusha mbingu
ili Mtatiro nionekane mwizi atakuwa anamwaga maji baharini tu. Nina makubaliano
ya kusimamia mambo makubwa maishani bila kujali nalipwa nini na bila kukubali
kuhongwa.
“Kambaya akaulize namna nilivyosaidia maelfu ya wanafunzi
wa vyuo vikuu vya Tanzania na wengine wakiwa hawana matumaini ya kupata mikopo
kabisa, awaulize namna walivyoniletea malaki ya fedha za shukrani na sikuwahi
kukubali kupokea hata senti tano yao. Tabia ya wizi ina minyororo yake na mimi
Mtatiro sikuwahi kufikiria kuwa mwizi,”alisema.
Alihoji kuhusu Sh milioni 369, alizomtuhumu Kambaya kuwa
alishiriki kuiba kimkakati kwa kusaidiana na Lipumba na kundi lao baada ya Januari
4 mwaka huu, ambapo Magdalena Sakaya, Thomas Malima na mwingine aliyetajwa kwa
jina moja la Zainab, walifanywa watia saini wa akaunti ya wilaya ya CUF.
Mtatiro alidai kuwa baada ya Kambaya na wenzake kuchukua
fedha hizo, walikwenda kwa Lipumba na kuanza kugawana, hivyo hapasawi
kuzifananisha fedha halali za chama zilizotumwa Igunga kwa awamu na fedha hizo
zilizochukuliwa Hazina kinyemela.
Mtatiro alisema wakati yeye anawekewa fedha zaidi ya Sh
milioni 100 katika akaunti yake, kulikuwa na baraka ya Kamati ya Utendaji ya
Taifa, Katibu Mkuu, Mwenyekiti Taifa na Kurugenzi ya Fedha kwa ajili ya kampeni
za Igunga.
Alisisistiza kuwa hakukuwa na nia yoyote mbaya kwa chama
kumwelekeza afungue akaunti na kisha kuiweka fedha kwa ajili ya bajeti ya
kampeni kwa awamu.
Mtatiro alisisitiza kuwa yeye ni mtu wa kanuni na kwamba
hawezi kuyumbishwa na wezi.
"Kimaadili mimi huwachukia wezi na waongo. Kwa sababu
tunayo nafasi ya kuchukua hatua kwa kila mwizi, Msajili wa Vyama vya Siasa,
Jaji Francis Mutungi, Bwaba Yule na wenzake. Hatua zitachukuliwa haraka
sana," alisema.
0 comments:
Post a Comment