Grace Gurisha
Mariam Mrita |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Januari 23
inatarajia kutoa uamuzi wa kumwacha au kutomwacha huru mjane wa bilionea Erasto
Msuya, Mariam Mrita (41) na mwenzake.
Hiyo inatyokana na upande wa Jamhuri kushindwa kurekebisha
hati ya mashitaka dhidi yake.
Uamuzi huo utatolewa na Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa
baada ya Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi na wakili wa utetezi, John Malya
kutoa hoja za kisheria kutokana na kwamba kila mmoja anavutia kwake.
Kishenyi alidai kuwa walishindwa kufanya marekebisho kama
Mahakama ilivyoamuru, kwa sababu muda wa siku mbili waliokuwa wamepewa ulikuwa mfupi,
kwa hiyo akaomba kupewa muda Zaidi, ili kurekebisha kwa kuwa suala la hati linahitaji
umakini.
Hata hivyo, Malya alidai kuwa amri iliyotolewa mahakamani
hapo ni ya kisheria, hivyo upande wa Jamhuri
ulitakiwa kutekeleza ama kukata rufaa, lakini ulishindwa kufanya hivyo.
Kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kutekeleza amri
hiyo, aliiomba Mahakama iwaache huru washitakiwa kwa sababu hakuna hati sahihi
ya mashitaka inayowafanya waendelee kushitakiwa.
Akijibu hoja hiyo, Mutalemwa alidai kuwa hawajashindwa
kuleta hati hiyo, lakini kama alivyosema awali kuwa anaomba muda zaidi na kutokana
na hilo, wataieleza Mahakama kama watakata rufaa au la.
Januari 9 Mahakama hiyo iliamuru upande wa Serikali
ubadilishe hati ya mashitaka ndani ya siku mbili ambapo alisema uamuzi huo ulitokana na kupitia hoja
za pande zote mbili na kubaini kuwa hati ya mashitaka ina upungufu sehemu mbili
ukiwamo wa kutoonesha kama kuna mtu aliyesababisha kifo cha mtu mwingine.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Miriam na Revocatus Muyela
wanadaiwa kumuua kwa makusudi dada wa bilionea, Msuya, Aneth Msuya kwa kumchinja
nyumbani kwake eneo la Kibada Kigamboni, Dar es Salaam Mei 25 mwaka jana.
Miriam ambaye ni mshitakiwa wa kwanza wa kesi hiyo ni
mjane wa bilionea Msuya ambaye aliuawa kwa risasi Agosti mwaka juzi Mijohoroni
kando ya barabara ya Arusha – Moshi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
0 comments:
Post a Comment