*Wamkumbuka siku chache baada ya kuondoka Ikulu
*Kiini
ni matamko na uamuzi wa kila siku ya Rais mpya
CALIFORNIA,
Marekani
Donald Trump |
CHINI ya siku 10 za urais wa Trump
inaonekana kwamba kila siku kunaibuka vita vipya na baadhi ya Wamarekani
wanamtaka Rais mstaafu Barack Obama aingilie kati.
“Vita dhidi ya ukweli. Vita dhidi ya
urais wa Mexico. Vita dhidi ya vyombo vya habari. Vita dhidi ya mazingira. Vita
dhidi ya NATO (Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Ulaya). Vita dhidi ya Waislamu.
“Vita dhidi ya Mfumo wetu wa Uchaguzi.
Vita dhidi ya nyota wa Hollywood. Vita dhidi ya haki za wanawake. Vita dhidi ya
China. Vita dhidi ya miiko ya Rais. Vita dhidi ya wakimbizi.” Anaandika Maclen
Zilber, Mwana Mikakati na Mshauri wa Masuala ya Kampeni wa Democrats aliyeko
Hollywood, California
Urais wa Obama una siku chache tu nje ya
Ikulu, na tayari maswali yameanza kuibuka juu ya kama vita hivi alivyovichochea
Trump vitakwisha.
Msimamo wa Rais huyu wa sasa wa
kuendelea ‘kumwaga petroli kwenye moto’ huku akionesha uhasama wa wazi wazi
duniani, nyumbani na kimataifa, unazidi kusababisha mvutano ndani na nje ya
Marekani, wakati akipanda mbegu ya mgogoro, vurugu na ghasia kwenye sayari hii.
Kwa kuelewa kabisa, Rais Obama aliweka
wazi kwamba atamfanyia wema Donald Trump kama ilivyofanywa na viongozi
waliomtangulia, atakaa kimya na kumruhusu Rais mpya aongoze nchi bila
kuingiliwa na mtangulizi wake, anasema Zilber.
Lakini kutokana na umaarufu alionao kwa
Wamarekani na watu wengine nje ya Taifa hili, hivi sasa ni muda mwafaka kwa
Rais Obama kuvunja taratibu na ukimya wake.
Kwa sasa, katika kipindi hiki cha kiza,
tunahitaji msemaji wetu mkuu wa Taifa letu, afute vumbi viatu vyake na arejee
uwanjani. Mtu ambaye alishawishi Taifa kuamini kwamba sisi si majimbo mekundu
wala bluu. Kijana mwembamba mwenye jina la kuvutia, ambaye kuna wakati
alitufanya tuamini katika matumaini na mabadiliko.
Kitu pekee kinachoweza kushinda hofu ni
matumaini. Rais Obama, tunajua umetoa kila kitu ulichokuwanacho kwa ajili yetu,
na hatuna haki yoyote ya kukutaka kujitolea maisha yako zaidi. Lakini
Wamarekani wanahitaji talanta zako, tunahitaji sauti yako, tunahitaji kalamu
yako ya unyoya, na tunahitaji uadilifu wako.
Ulisema mara ya mwisho, kwamba ungeweza
kumshinda Donald Trump kama ungeshindana naye moja kwa moja. Ni muda sasa wa
kuthibitisha hilo.
Vitendo vya Trump vinaibua maswali zaidi
juu ya kama hatua zake hatari na za ubaguzi zinawaweka Wamarekani na binadamu
wote wa Dunia hii, kwenye mwelekeo wa mgongano ambao unaweza kusababisha vita
vya dunia.
Kwenye kiini ambacho kinaufanya urais wa
Trump kuwa wa hatari zaidi ni nia yake ya wazi ya kuwaona Wamarekani kama watu
wanaoweza kudanganyika kirahisi.
Mara ya kwanza Trump alifanya hivyo kupitia
kwa Msemaji wa Ikulu, Sean Spicer, kuhusu umati uliohudhuria kuapishwa kwake.
Akafanya hivyo tena kesho yake alipokwenda makao makuu ya Idara ya Ujasusi
(CIA), akieneza upotoshaji kama alivyofanya Spicer.
Katika tukio hilo hilo, Trump alipotosha
ukweli juu ya uhusiano wake na taasisi hiyo ya intelijensia, akisema vyombo vya
habari vilitengeneza uzushi kwamba ana uhusiano mbaya na chombo hicho, ambapo
siku chache kabla ya kuapishwa kwake alikifananisha na “Ujerumani ya Wanazi,”
Siku iliyofuata, na siku ya tatu ya
urais wake, mshauri wake mwandamizi, Kellyanne Conway alikataa kukanusha uongo
wa Trump, na badala yake akauita “ukweli mbadala,” kwenye kipindi cha NBC cha
Meet the Press (Kutana na Waandishi).
Mbaya zaidi, siku ya nne, baada ya
kuapishwa kuwa amirijeshi mkuu wa 45 wa Marekani, Trump aliwadanganya viongozi
wa Bunge la Congress, akisema kulikuwa na udanganyifu mkubwa wa upigaji kura kiasi
cha kura hewa kati ya milioni 3 na 5 kwenye uchaguzi wa Novemba 16.
Madai hayo ya uongo kimsingi yalishusha
uhalali wa uchaguzi wake kama Rais wa Marekani, lakini pia mfumo mzima
unaounganisha pamoja demokrasia yetu ya uwakilishi.
Uongo huu umejikita zaidi kwenye nini
kinachotarajiwa kutokea katika miaka kadhaa ijayo ya utawala wa Trump na kwa bahati
mbaya, tabia yake ya udikteta, ukichaa na ukurupukaji, imeongeza kuuweka
hatarini usalama wa kila Mmarekani.
Fikiria. Kama Trump anapenda kuendelea
na uongozi wake usio na msingi juu ya uchaguzi wake mwenyewe, baada ya madai
yake ya kuwapo udanganyifu kupingwa au idadi ya watu waliohudhuruia sherehe zake za
kuapishwa kutokana na hisia zake za kutaka kuonekana bora zaidi pamoja na
udhaifu alionao, ni nini kitamzuia kudanganya juu ya mgogoro wa kidunia utakaoliweka
Taifa letu kwenye sintofahamu?
Hatua kama hiyo itasababisha vita, umwagaji
damu na hata upotevu wa maisha ya Wamarekani – na hatutaweza hata kujua kama
anaweza kuamini visingizio vinavyosemwa kuhusu vita hivyo.
Zaidi ya uongo wake usio na soni, nguvu
zake nyepesi za kalamu azitumiazo kusaini maagizo ya utendaji au maandiko yake
kwenye mitandao ya kijamii, ya kibaguzi kwa viongozi wengine wa dunia,
zinasababisha sintofahamu na mabadiliko makubwa duniani - na havionekani
kumshitua au hata washauri wake hata kidogo.
Mambo yote haya yanaonekana kuubainisha
ukweli, kwamba kila siku inayopita, ukosefu wa utulivu unachemka chini kwa
chini duniani na maumivu yanazidi kuongezeka ndani ya Marekani yakiongozwa na
kiongozi wetu mfitini, Donald Trump.
Ulisema mara ya mwisho, kwamba ungeweza
kumshinda Donald Trump kama ungeshindana naye moja kwa moja. Ni muda sasa wa
kuthibitisha hilo.
0 comments:
Post a Comment