Mwandishi Wetu
Baraza la Mawaziri |
TANZANIA imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 20 bora duniani kwa
kuwa na sehemu kubwa ya mawaziri wanawake kwenye Baraza la Mawaziri, huku
ikishika nafasi ya tano Afrika.
Mtandao wa How Africa, The Rise of Africa, umeeleza hilo
jana ukinukuu utafiti mpya ulioandaliwa na taasisi ya UN Women na Inter
Parliamentary Union, ambazo zinaongoza duniani kwa kupigania ajenda ya kuongeza
uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya uamuzi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Cape Verde ndiyo nchi
inayoongoza kwa kuwa na sehemu kubwa ya wanawake kwenye Baraza la Mawaziri,
inayoundwa na wanawake ambalo kati ya mawaziri wote 17, tisa ni wanawake.
Mbali na kuwa ya kwanza Afrika, Cape Verde imetajwa kuwa
ya pili duniani kwa kigezo hicho, ikitanguliwa na Finland, ambayo ndiyo ya
kwanza duniani kwani kati ya mawaziri wake 16, mawaziri 10 ni wanawake.
Nchi ya pili Afrika kwa kuwa na sehemu kubwa ya wanawake
kwenye Baraza la Mawaziri ni Afrika Kusini, ambayo kati ya mawaziri 36,
mawaziri 15 ni wanawake.
Rwanda inashika nafasi ya tatu Afrika, kwani kati ya
mawaziri wake 31, mawaziri 11 ni wanawake na inafuatiwa na Burundi na Tanzania
katika nafasi ya tano.
Tanzania
Baraza la Mawaziri Tanzania likijumuisha na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, lina mawaziri 36 na kati yao, tisa ni wanawake.
Mawaziri hao ni Jenista Mhagama (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu); Ummy
Mwalimu (Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto); Anjela Kairuki (Utumishi na Utawala Bora); Profesa Joyce Ndalichako (Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi).
Wengine ni Dk Ashantu
Kijaji (Naibu Fedha na Mipango); Dk
Susan Kolimba (Naibu Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afika Mashariki); Angelina Mabula (Naibu Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi); Stella
Manyanya (Naibu Elimu, Sayansi Teknolojia na
Ufundi) na Anastasia
Wambura (Naibu Habari, Utamaduni, Wasanii na
Michezo).
Nchi zingine
Afrika sasa ina nchi saba
ambazo angalau asilimia 30 ya mawaziri wao ni wanawake na katika nchi 30
duniani zinazofikia wingi huo wa mawaziri wanawake na kuzidi, robo ya nchi hizo
zinatoka Afrika na kufanya Bara hilo kuwa la pili kwa kufikia kigezo hicho baada
ya Ulaya.
Nchi yenye uchumi mkubwa
zaidi Afrika; Nigeria kati ya mawaziri 29, saba ni wanawake uwiano sawa na Jamhuri
ya Afrika ya Kati, ambayo kati ya mawaziri 22,
watano ni wanawake.
Djibouti ndiyo ya mwisho, ambayo kati ya mawaziri wake
19, waziri mmoja tu ndiye mwanamke, wakati Sierra Leone ina mawaziri wanawake
wawili tu kati ya mawaziri 29.
Bungeni
Rwanda inaongoza duniani katika uwakilishi wa wanawake bungeni
ambapo kati ya viti 80 vya ubunge, viti 51 ni vya wanawake sawa na asilimia 63
ya wabunge wote.
Ushelisheli, Senegal na Afrika Kusini zinafuata na kuwa
miongoni mwa nchi 10 bora duniani kwa kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake bungeni.
Msumbiji, Angola, Tanzania, Algeria, Zimbabwe, Tunisia, Kameruni
na Burundi, ni miongoni mwa nchi zingine za Afrika, zenye zaidi ya asilimia 30
ya wabunge wanawake kwenye mabunge yao.
Nchi zenye uwakilishi mbovu wa wanawake bungeni ni Swaziland, Nigeria, Congo zote mbili, Ivory Coast,
Gambia, Mali na Botswana, ambazo uwakilishi wa wanawake kwenye mabunge yao ni
chini ya asilimia 10.
Wastani wa uwakilishi wa wanawake kwenye mabunge ya nchi za
Kusini mwa Jangwa la Sahara, umetajwa kuwa asilimia 22.4 katika mataifa yenye
mabunge yenye sehemu moja na asilimia 20 kwa mabunge yenye sehemu mbili; Bunge
la Wawakilishi na Bunge la Seneti.
0 comments:
Post a Comment